Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda akiwa katika picha ya pamoja na Mwanariadha Sajinitaji Alphonce Simbu wakati akiwasilisha medali ya dhahabu aliyeshinda katika mbio ndefu za Marathon kwenye Mashindano ya Dunia (WAC 2025) yaliyofanyika Septemba 15, 2025, jijini Tokyo, Japan.
……
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania (CDF), Jenerali Jacob John Mkunda, amewapongeza wanamichezo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), akiwemo mwanariadha Sajinitaji Alphonce Simbu, kwa mafanikio makubwa waliyopata katika mashindano ya kitaifa na kimataifa mwaka 2025.
Sajinitaji Simbu alitwaa medali ya dhahabu katika mbio ndefu za Marathon kwenye Mashindano ya Dunia (WAC 2025) yaliyofanyika Septemba 15, 2025, jijini Tokyo, Japan. Ushindi huo umeweka historia kwa Tanzania kwa kuwa mara ya kwanza kwa mwanariadha wa kijeshi kushinda katika kiwango hicho cha kimataifa.
Aidha, Jenerali Mkunda amewapongeza timu ya mpira wa miguu ya wanawake ya JKT Queens kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) mwaka 2025 yaliyofanyika Nairobi, Kenya. Pia, ameipongeza Kanda ya Ngome kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya michezo mbalimbali ya Majeshi (BAMMATA) yaliyofanyika Zanzibar.
Akizungumza katika hafla fupi ya pongezi na makabidhiano ya makombe na medali iliyofanyika Septemba 25, 2025, katika Viwanja vya Lugalo Golf, Dar es Salaam, Jenerali Mkunda amesema kuwa ushindi huo umeipa heshima kubwa JWTZ na Tanzania kwa ujumla.
“Ushindi wa Sajinitaji Simbu ni fahari kubwa kwa Jeshi letu. Ameonyesha uzalendo, bidii na nidhamu kwa kuweka malengo na kuyatimiza,” amesema Jenerali Mkunda.
Kuhusu mafanikio ya JKT Queens, CDF Mkunda ameeleza kuwa timu hiyo imetwaa taji hilo kwa mara ya pili, mara ya kwanza ikiwa mwaka 2023 jijini Kampala, Uganda, na mara ya pili mwaka huu wa 2025.
Amesitiza kuwa Makao Makuu ya Jeshi yanaendelea kuweka kipaumbele katika kukuza michezo na kuendeleza vipaji kwa wanajeshi na vijana kwa ujumla.
“Michezo ni sehemu ya kazi jeshini. Mafanikio haya yanatoa hamasa kwa wanajeshi na vijana wa Kitanzania kuwa na nidhamu, juhudi na kujituma katika kila jambo,” ameongeza
Naye Mkuu wa Operesheni na Mafunzo wa JWTZ, Meja Jenerali Ibrahim Michael Mhona, amesema kuwa Jeshi linaendelea kuandaa wanamichezo bora na wenye ushindani mkubwa kwa ajili ya mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Meja Jenerali Mhona amewapongeza wanamichezo wote wa JWTZ na JKT kwa mafanikio yao katika mwaka huu wa 2025, huku akieleza kuwa juhudi zao ni mfano bora wa uzalendo na bidii ya kazi.