Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akizungumza leo, Septemba 27, 2025 wakati akifungua Mkutano wa Mwaka wa Jumuiya ya Ahmadiyya Muslim Tanzania uliofanyika katika Ukumbi wa Msikiti wa Ahmadiyya uliopo Kata ya Msongola, Mtaa wa Mvuleni, Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (kulia) akizungumza jambo na Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania, Sheikh Khawaja.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Ahmadiyya Muslim Tanzania.
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akiangalia maonesho ya kazi mbalimbali zinazofanywa na Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania.
……….
Serikali kupitia Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imesema itaendelea kuhakikisha kuwa haki za binadamu zinalindwa kwa mujibu wa Katiba, Sheria za nchi pamoja na Mikataba mbalimbali ya Kimataifa ambayo Tanzania imeridhia.
Akizungumza leo, Septemba 27, 2025, jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Jumuiya ya Ahmadiyya Muslim Tanzania, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Mhe. Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, amesema kuwa jitihada za Tume zinalenga kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapata haki zake bila ubaguzi wowote, ikiwa ni pamoja na usawa mbele ya sheria.
Jaji Mstaafu Mwaimu amebainisha kuwa haki mbalimbali kama vile upatikanaji wa elimu bora, huduma ya maji safi, mazingira salama, uhuru wa kutoa maoni, ajira, uhuru wa vyama vya siasa, pamoja na haki za wanawake, watoto na watu wenye ulemavu ni kati ya maeneo ambayo Tume inayaangazia kwa umakini, kwa kuwa ni nguzo muhimu za maendeleo ya Taifa.
“Misingi ya haki iliyowekwa ndani ya Katiba na sheria zetu inalenga pia kulinda usalama wa taifa na umma, kuzuia machafuko, kudumisha maadili ya jamii na kulinda haki za wengine, hususan uhuru wa mtu binafsi,” ameaema Jaji Mwaimu.
Aidha, Jaji Mwaimu ameeleza kufurahishwa kwake na kazi nzuri zinazofanywa na Jumuiya ya Ahmadiyya katika kuendeleza misingi ya amani, upendo, mshikamano, kuhimiza utii wa sheria, maadili mema kupitia mafundisho ya dini ya Kiislamu pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii.
Amesisitiza kuwa haki ya kuabudu ni miongoni mwa haki za msingi zinazolindwa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ibara ya 19 ya Katiba hiyo inatoa uhuru kwa kila mtu kuamini, kuabudu na kushiriki katika dini au imani anayoichagua bila kulazimishwa au kubaguliwa.
Kwa upande wake, Amir na Mbashiri Mkuu wa Jumuiya ya Waislamu wa Ahmadiyya Tanzania, Sheikh Khawaja Muzafar Ahmad, ameipongeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa kazi kubwa na ya kuigwa inayofanywa katika kusimamia haki, usawa na utawala bora nchini.
Sheikh Ahmad ameeleza kuwa miongoni mwa majukumu makuu ya Jumuiya yao ni kueneza amani, upendo, mshikamano, kuhimiza utii wa sheria, kuendeleza maadili mema kupitia mafundisho ya dini ya Kiislamu pamoja na kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa watanzania bila kujali itikadi au tofauti za kidini.