Na.Sophia Kingimali.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umebuni mbinu za kutumia teknolojia mbadala katika ujenzi wa barabara na madaraja, hatua iliyosaidia kuokoa mabilioni ya shilingi za serikali na kuharakisha utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini.
Pia,TARURA inatarajia kujenga daraja kubwa kuliko yote jijini Dar es salaam ambalo litatumia zaidi ya bilioni 1.6
Akizungumza leo Septemba 26,2025 jijini Dar es salaam Mratibu wa Ujenzi kwa Teknolojia Mbadala wa TARURA, Phares Ngeleja, amesema serikali imeikabidhi TARURA jukumu la kusimamia, kujenga na kukarabati mtandao wa barabara wenye urefu wa takribani kilomita 144,429.77 kote nchini.
“Ujenzi na ukarabati wa barabara unahitaji fedha nyingi sana. Ndiyo maana TARURA tumeamua kutafuta njia nafuu zaidi ambazo zitawasaidia wananchi kupata barabara na madaraja kwa gharama ndogo lakini zenye ubora unaokubalika,” amesema Ngeleja.
Ngeleja amesema madaraja ni kiungo muhimu katika barabara yoyote, hivyo TARURA imeweka mkazo mkubwa katika ujenzi wake.
“Mpaka sasa tumeshakamilisha madaraja 453 kwa gharama ya shilingi bilioni 32. Kama tungetumia zege, tungehitaji zaidi ya shilingi bilioni 117. Hii ina maana tumesaidia serikali kuokoa fedha nyingi,” alieleza.
Aidha, amebainisha kuwa miradi hiyo imetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, huku ikitarajiwa kujengwa daraja refu zaidi jijini Dar es Salaam.
“Tunapanga kujenga daraja katika eneo la Mwanagati–Majohe, Mto Mzinga. Daraja hili litagharimu shilingi bilioni 1.6 na litakuwa msaada mkubwa kwa wakazi wanaosafiri kuelekea katikati ya jiji,” alisema.
Mbali na madaraja, TARURA pia inajenga barabara za mawe katika mikoa ya Mwanza, Kigoma, Rukwa na Morogoro.
Kwa mujibu wa Ngeleja, jumla ya kilomita 29.54 zimekamilika kwa gharama ya shilingi bilioni 14.
“Kama tungetumia kiwango cha double surface gharama zingefika bilioni 19, na kama tungetumia lami nzito zingepanda hadi bilioni 33. Hii ni njia bora ya kupunguza gharama,” alisema.
Kwa upande wake, Mhandisi Ephraim Kalunde, Msimamizi wa Mradi wa Rural and Urban Access Improvement Project (RISE) kutoka makao makuu ya TARURA, amesema mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia ambapo mradi huo ulianza Novemba 2021 na unatarajiwa kukamilika Juni 2027. Huku ukitekelezwa katika wilaya kadhaa zikiwemo Iringa, Handeni (Tanga), Luagwa na Mbogwe (Geita).
“Moja ya vipengele muhimu ni kuboresha barabara kutoka tambarare kwenda kiwango cha lami. Pia tunajenga vivuko kuondoa vikwazo vinavyowazuia wananchi kufika kwenye huduma za kijamii,” alisema Kalunde na kuongeza kuwa hadi sasa, utekelezaji wa kipengele cha vivuko umefikia asilimia 95, ambapo zaidi ya kilomita 2,010 kati ya 2,227 zimerudishiwa mawasiliano.
“Kupitia uboreshaji huu, zaidi ya wananchi milioni 2.69 wameweza kufikiwa na huduma muhimu, huku kata na vijiji vingi vikifunguliwa fursa za kiuchumi,” amesema.
Miradi hii ya TARURA inatajwa kuwa chachu ya maendeleo, hasa vijijini, kwani inarahisisha usafirishaji wa mazao, upatikanaji wa huduma za afya na elimu, na kuchochea ukuaji wa pato la wananchi.