Geita
Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA) limepokea mwaliko rasmi kutoka kwa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Malawi kushiriki katika Maonesho ya Kwanza ya Teknolojia ya Madini nchini humo, yanayotarajiwa kufanyika Novemba 2025.
Mwaliko huo umetolewa na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Malawi, Bw. Percy Maleta, wakati wa kikao maalum kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Lenny Hotel mkoani Geita, sambamba na Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea kaika viwanja vya Samia Suluhu Hassan Bombambili mkoani Geita.
Akizungumza katika kikao hicho, Bw. Maleta amesema kuwa Malawi ina utajiri mkubwa wa rasilimali za madini, lakini bado kuna changamoto ya teknolojia duni, ukosefu wa mitaji, elimu ya madini na utafiti. Amesisitiza kuwa ushirikiano na FEMATA unaweza kusaidia kuimarisha sekta hiyo kwa pande zote mbili kwa kubadilishana uzoefu na maarifa.
“Malawi ina fursa nyingi kwenye Sekta ya Madini, lakini bado tunahitaji kujifunza kutoka kwa wenzetu wa Tanzania, hasa katika matumizi ya teknolojia na mifumo bora ya usimamizi,” amsema Maleta.
Katika ziara yao, ujumbe kutoka Malawi umetembelea Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini 2025 mkoani Geita na kujionea namna Tanzania inavyotekeleza shughuli za sekta hiyo, hususan katika kuhamasisha matumizi ya teknolojia na ushiriki wa wachimbaji wadogo.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa FEMATA, Katibu wa Wachimbaji Madini wa Mkoa wa Shinyanga (SHILEMA) Gregory Kibusi ameeleza kuwa FEMATA ipo tayari kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Malawi katika maeneo mbalimbali ya maendeleo ya Sekta ya Madini, kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuchochea maendeleo endelevu ya uchumi wa nchi zote mbili.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martin Shigella, amekutana na ujumbe huo wa Malawi na kushiriki nao katika chakula cha pamoja. Mhe. Shigella ameukaribisha ujumbe huo mkoani humo na kupongeza juhudi za kujifunza kutoka kwa Tanzania katika usimamizi wa mifumo ya Sekta ya Madini.