NA JOHN BUKUKU- PWANI
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Serikali imejipanga kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi ili kuwawezesha wananchi wa kipato cha chini kujenga nyumba bora na za kisasa kwa bei nafuu.
Akihutubia wananchi wa Mkoa wa Pwani katika muendelezo wa kampeni za CCM, Dkt. Samia amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata makazi bora na salama bila kubebeshwa gharama kubwa zinazozuia ndoto za kumiliki nyumba za kisasa.
Amesema kupunguza gharama za vifaa vya ujenzi ni sehemu ya ajenda ya kitaifa ya makazi bora ambayo imekuwa ikitekelezwa kwa vitendo katika maeneo mbalimbali, huku Mkoa wa Pwani ukiendelea kuwa mfano wa mafanikio makubwa kwenye sekta hiyo.
“Tunataka kuona wananchi, hasa wa kipato cha chini, wanajenga nyumba bora, za kisasa na kwa gharama nafuu. Serikali imejipanga kushusha gharama za vifaa vya ujenzi ili kila mmoja aweze kufanikisha ndoto hii,” amesema Dkt. Samia.
Vilevile, amewataka wananchi kuendelea kuiamini CCM na kuipa ridhaa ya kuongoza katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, ili iweze kutekeleza kwa ufanisi mpango huo mkubwa wa kitaifa na kuhakikisha makazi bora kwa Watanzania wote.