NA JOHN BUKUKU – PANGANI, TANGA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni zake Septemba 29, 2025 wilayani Pangani, mkoani Tanga, akisisitiza dhamira ya serikali kuimarisha sekta ya uvuvi kwa maendeleo ya wavuvi na jamii zinazotegemea bahari.
Dkt. Samia amesema serikali ya CCM tayari imewezesha upatikanaji wa boti 15 za kisasa zinazotumika katika shughuli za uvuvi wa samaki na dagaa, hatua inayolenga kuongeza uzalishaji na kipato cha wavuvi wadogo. Amesema hatua hiyo itakwenda sambamba na ujenzi wa soko kubwa la kisasa la samaki lenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.3, ambalo litakuwa chachu ya kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi na ajira mpya kwa wananchi wa Pangani na maeneo mengine.
Aidha, Dkt. Samia ameeleza kuwa mpango huo wa serikali unalenga si tu kuongeza tija kwenye sekta ya uvuvi, bali pia kuhakikisha wavuvi wanapata masoko ya uhakika na miundombinu ya kisasa itakayowawezesha kushindana kibiashara ndani na nje ya nchi.
Amesema serikali itaendelea kutoa mikopo kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, ambapo zaidi ya shilingi milioni 642 tayari zimetolewa, huku akibainisha kuwepo kwa mfuko maalumu wa kusaidia wafanyabiashara wadogo wadogo, wakiwemo wavuvi wadogo na wafanyabiashara wa mazao ya baharini.
Kwa mujibu wa Dkt. Samia, sekta ya uvuvi itaunganishwa na mipango ya viwanda vitakavyoanzishwa katika wilaya mbalimbali, ili kuongeza thamani ya samaki na mazao mengine ya baharini, na hivyo kutoa fursa zaidi za ajira kwa vijana na kuongeza kipato cha kaya zao.