
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema iwapo atapewa ridhaa ya kuunda serikali katika uchaguzi mkuu ujao wa Oktoba 29, 2025, serikali yake itatekeleza ujenzi wa barabara ya Kibaha–Chalinze–Morogoro kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Akizungumza Jumapili, Septemba 28, 2025, kwenye viwanja vya Polisi, Chalinze, Dkt. Samia amesema barabara hiyo ni ya kimkakati kiuchumi, hivyo ushirikiano na sekta binafsi utatoa nafasi kwa serikali kuelekeza rasilimali katika maeneo mengine ya kipaumbele.
“Hii ni barabara yenye tija kiuchumi, hivyo tutashirikiana na sekta binafsi ili wao watoe fedha sisi tufanye mambo mengine,” amesema Dkt. Samia.
Katika sekta ya afya, Dkt. Samia ameahidi kuendeleza maboresho katika Hospitali ya Wilaya ya Chalinze ili iwe na hadhi stahiki na kutoa huduma zote muhimu. Pia aliwapongeza wakazi wa eneo hilo kwa kufanikisha kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Vilevile, ameahidi ujenzi wa shule mpya za msingi katika maeneo ya Chaua, Kibindu, Zigua na Changalikwa, sambamba na kuendeleza mpango wa elimu bila ada. Ameongeza kuwa serikali yake itatekeleza mpango wa bima ya afya kwa wote, ambapo majaribio yataanza ndani ya siku 100 za kwanza iwapo atachaguliwa.
STORI NA ELVAN STAMBULI, GPL