Na John Bukuku – Tanga
Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeendesha kampeni maalum ya elimu ya mionzi kwa wanafunzi wa shule za sekondari mkoani Tanga, ambapo jumla ya wanafunzi 9,391 kutoka shule 10 walipata mafunzo hayo ndani ya wiki moja, kuanzia Septemba 22 hadi 26, 2025.
Shule zilizofikiwa ni pamoja na Chumbageni, Galanosi, Kiomoni, Mikanjuni, Mkwakwani, Usagara, Nguvumali, Pongwe, Mabokweni na Msambweni. Kupitia semina, mijadala ya papo kwa papo, mafunzo ya vitendo na maonesho ya vifaa vya mionzi, wanafunzi walipata uelewa mpana kuhusu matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia na mchango wake katika maisha ya kila siku.
Kwa muda mrefu, teknolojia ya nyuklia imekuwa ikihusishwa zaidi na hofu ya silaha za maangamizi. Hata hivyo, TAEC imeweka mkazo mkubwa katika kuelimisha vijana kuwa mionzi na teknolojia ya nyuklia vina mchango mkubwa katika sekta za afya, kilimo, viwanda na mazingira.
Miongoni mwa faida zilizotajwa ni pamoja na kutibu na kuchunguza magonjwa sugu kama saratani kupitia tiba ya mionzi (radiotherapy), kuboresha mbegu za kilimo, kusafisha maji, na kuongeza ubora wa bidhaa za viwandani.
Aidha, TAEC inalenga kupitia elimu hiyo kuhamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi hususan Fizikia, Kemia, Baiolojia na Hisabati, ambayo ni msingi wa taaluma zinazohusiana na fizikia tiba, usalama wa mionzi na uhandisi wa nyuklia.
Kwa mujibu wa TAEC, kampeni hiyo inalenga pia kulinda usalama wa jamii na mazingira, sambamba na kuandaa wataalamu wa baadaye watakaosaidia taifa katika mapambano dhidi ya saratani na changamoto nyingine zinazohitaji matumizi ya teknolojia ya mionzi.