Mnamo Septemba 14, 2025 liliripotiwa tukio la kutekwa nyara kwa Shyrose Michael Mabula [21] aliyekuwa mwanachuo mwaka wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Mzumbe ndaki ya Mbeya Kitivo cha Sheria na watu wasiofahamika, ambapo Septemba 16, 2025 saa 5:00 usiku huko Mtaa wa Morovian uliopo Kata ya Isyesye Jijini Mbeya mwili wa mwanachuo huyo ulikutwa ukiwa umechomwa moto.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilianza ufuatiliaji ili kuwabaini na kuwakamata waliohusika katika tukio hilo na Septemba 24, 2025 saa 4:00 asubuhi alikamatwa Marwa Nyahega John [25] mkazi wa Uzunguni “A” Mbeya ambaye katika mahojiano alikiri kuwa yeye pamoja na wenzake wawili ambao ni Edward Christopher Kayuni na Websta William Mwantebele kwa pamoja walikula njama na kumteka nyara Shyrose Michael Mabula [ambaye kwa sasa ni marehemu] kwa lengo la kujipatia fedha nyingi kutoka kwa baba yake mzazi aitwaye Dkt. Mabula Michael.
Baada ya kumteka walianza kupiga simu kwa familia yake kwa lengo la kujipatia fedha na iliposhindikana kupata fedha hizo kwa kuhofia kwamba watakamatwa walipanga kumuua binti huyo ili kupoteza ushahidi.
Awali walimnywesha sumu ambayo ni dawa ya kuulia magugu mashambani aina ya “Round Up” iliposhindikana kuondoa uhai wake waliamua kumnyonga kwa kamba hadi kufa kisha kuuchoma moto mwili wake.
Baada ya kupata taarifa hiyo ufuatiliaji uliendelea na Septemba 25, 2025 alikamatwa mtuhumiwa Websta William Mwantebele [27] Mlinzi ambaye alikiri kushiriki kufanya tukio la utekaji na mauaji ya binti huyo na kueleza kuwa tukio hilo walifanya kwa kushirikiana na wenzake ambao ni Marwa Nyahega John na Edward Christopher Kayuni.
Aidha alieleza kuwa anaweza kwenda kuwaonyesha Askari watuhumiwa wenzake kwani wamepanga kwenda mafichoni kwenye machimbo yaliyopo Wilayani Chunya.
Septemba 27, 2025 aliwapeleka Askari Polisi katika Kijiji cha Chalangwa eneo walilokuwa wamepanga kukutana.
Askari Polisi waliweka mtego kwa ajili ya kumkamata mtu ambaye Websta William Mwantebele [Mtuhumiwa] atawaonyesha. Baada ya muda alifika mtu mmoja na mtuhumiwa huyo akawaeleza Askari kuwa huyo anayekuja ndiye Edward Christopher Kayuni waliyeshirikiana naye kumuua binti huyo.
Askari walipojaribu kumkamata mtuhumiwa huyo alichomoa kisu ghafla na kuanza kuwatishia Askari kwa kuwachoma kwa kisu hicho.
Askari walifyatua risasi hewani na kumuonya mtuhumiwa ajisalimishe na aache kitendo chake anachofanya lakini alikaidi amri na kumkunja shati Askari ndipo Askari mmoja alifyatua risasi iliyompata kwenye mguu wa kushoto na kuanguka chini.
Wakati purukushani hizo zikiendelea mtuhumiwa Websta William Mwantebele naye alianza kukimbia ili kukwepa mkono wa sheria dhidi yake ndipo Askari walimkimbiza huku wakipiga risasi hewani zaidi ya tatu na kumtaka asimame lakini alikaidi na kuendelea kukimbia kuelekea vichakani na ndipo alipompiga risasi zilizomjeruhi mguu wa kulia na mgongoni na kuanguka chini.
Majeruhi hao wote wawili walikimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Chunya kwa ajili ya matibabu lakini walipofikishwa walibainika kuwa wote wawili wamefariki dunia.
Aidha, katika ufuatiliaji zaidi wa tukio hili mtuhumiwa Marwa Nyahega John alieleza kuwa wakati wakimpa mateso Shyrose Michael Mabula na kumrekodi picha mjengeo na kumtumia baba yake ili atoe fedha nyingi, alimkata binti huyo kidole cha mkono wa kulia na baada ya mauaji hayo kidole hicho pamoja na nguo zake za ndani alizipeleka kwa mganga wa jadi huko maeneo ya Isyesye Jijini Mbeya kwa ajili ya kuwafanyia zindiko ili wasibainike na wala wasikamatwe na Polisi.
Mtuhumiwa huyo alikubali kwenda kuwaonyesha Askari kwa Mganga huyo alipopeleka kidole cha marehemu pamoja na nguo za ndani. Wakiwa njiani mtuhumiwa Marwa Nyahega John alikurupuka na kujirusha chini kutoka kwenye gari kitendo kilichopelekea kupata jeraha kubwa kichwani. Alikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ndipo ilibainika amefariki.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea na msako mkali kuwatafuta na kuwakamata watuhumiwa wengine akiwepo mganga wa jadi.
Katika upekuzi watuhumiwa hao walikutwa na pingu mbili, vitambulisho viwili vya bandia vya Jeshi la Wananchi Tanzania (TPDF) vyenye picha na majina yao, simu mbili zenye picha zinazoonyesha namna wanavyotekeleza uhalifu wa utekaji, na taarifa nyingine za mawasiliano baina yao kabla, wakati na baada ya kumteka nyara na kumuua Shyrose Michael Mabula.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa jamii, hasa vijana ambao wamepata mafunzo mbalimbali kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi yetu, wawe wazalendo na watumie mafunzo hayo kwa mujibu wa sheria na taratibu na siyo kutumia mafunzo hayo kufanya vitendo vya uhalifu.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa rai kwa baadhi ya wananchi kuacha tamaa ya kujipatia mali na fedha kwa njia haramu na badala yake wafanye kazi halali kwa ajili ya kujipatia kipato kwani uhalifu haulipi na hauna nafasi katika jamii. Wakumbuke wakifanya uhalifu wowote ule lazima mkono wa sheria utawafikia wakati wowote ule.