Na Pamela Mollel,Arusha
Katika kuadhimisha Siku ya Wazee Duniani 2025, wazee wa jiji la Arusha wamefanya mazoezi ya jogging yaliyokuwa kivutio kikubwa katika mitaa mbalimbali ya kata ya Olasiti mnamo tarehe 27 Septemba 2025.
Baada ya zoezi hilo la jogging, wazee waliendelea na mazoezi ya viungo yaliyolenga kuwafanya wawe na miili imara na yenye afya. Zoezi hilo liliendeshwa na Afisa Utamaduni wa Jiji la Arusha, Benson Maneno, ambaye alisisitiza umuhimu wa mazoezi kwa afya ya wazee.
Akizungumza wakati wa mazoezi hayo, Benson Maneno alisema lengo ni kuhamasisha wazee kuendelea kujali afya zao kupitia michezo na mazoezi ya mwili.
Wazee walioshiriki walitoa pongezi kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kuandaa shughuli hiyo na kuomba iendelee kufanyika mara kwa mara, wakisema itachangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha afya na ustawi wao.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ilikuwa:“WAZEE TUSHIRIKI UCHAGUZI KWA USTAWI WA JAMII YETU.”.