Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi nchini (PSPTB) imefanya tathmini ya bajeti na kuweka mikakati mipya ya kuboresha utendaji kazi kwa mwaka wa fedha 2025/2026, lengo likiwa kuongeza ufanisi katika sekta ya ununuzi na ugavi.
Akizungumza katika kikao kazi cha Baraza la Wafanyakazi kilichofanyika mkoani Morogoro, Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Bw. Godfred Mbanyi, amesema kikao hicho kimekuwa fursa ya kupitia utekelezaji wa malengo ya mwaka uliopita na kupanga mikakati mipya ya kufanikisha malengo ya mwaka ujao.
“Kikao hiki kinaangalia kwa mwaka uliopita wa fedha tulipanga kufanya nini na tumeweza kufanya kitu gani. Pia kinatupa nafasi ya kutathmini wapi tumefanya vizuri, wapi tumekwama na ni maeneo yapi yamebaki bila kutekelezwa. Hii itatusaidia kama taasisi kuweka mikakati mipya ya kuboresha utendaji katika mwaka wa fedha 2025/2026,” amesema Bw. Mbanyi.
Aidha amesema Mageuzi ya TEHAMA yamekuwa chachu ya kurahisisha mchakato wa usajili na mitihani ya kitaaluma, tofauti na awali ambapo kulikuwa na mlolongo mrefu wa urasimu, hadi sasa, bodi imefanikiwa kusajili zaidi ya wataalam 10,000, huku mwaka 2024 jumla ya wanafunzi 680 walifanyiwa mitihani ya kitaaluma, ikilinganishwa na lengo la wanafunzi 750.
“Bodi yetu inaendesha mitihani ya kitaaluma ya ununuzi na ugavi kwa wahitimu wa vyuo vikuu. Mitihani hii huwapa nafasi ya kupata vyeti vya kitaaluma vinavyowawezesha kufanya kazi kwa ufanisi na kwa weledi katika taaluma hii,” ameongeza Bw. Mbanyi.
Kwa upande wake, Katibu wa TUGHE tawi la PSPTB, Bi. Faraja Mgulambwa, amesema kikao kazi hicho ni jukwaa muhimu kwa wafanyakazi kwani kinawawezesha kutoa maoni yao, kushirikiana na menejimenti, na kutafuta suluhu za changamoto zinazowakabili.
“Tumekutana hapa mkoani Morogoro kwa siku mbili katika kikao kazi kinachotupa mwanga wa kujadili mambo mbalimbali ya taasisi yetu na kutafuta suluhu za changamoto za kazi,” amesema Bi. Mgulambwa.