Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imekuja na mkakati wa kupata taarifa sahihi na kwa haraka kupitia Mfumo wa Kieletroniki wa Ukusanyaji wa Taarifa za Matukio ya Wanyamapori Wakali na Waharibifu (Problem Animals Information System – PAIS) ili kusaidia upatikanaji wa taarifa sahihi za matukio ya wanyama hao kwa haraka.
Akifungua mafunzo ya mfumo huo kwa Maafisa Ugani 120 Jijini Dodoma kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Alexander Lobora, Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori amesema kuwa lengo la Serikali kuhifadhi rasilimali za wanyamapori ni kuleta maendeleo kwa Taifa na ustawi wa wananchi wake na si kugeuka kuwa mzigo kwa jamii.
“Miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na matukio ya mara kwa mara ya wanyamapori wakali na waharibifu ambayo imepelekea madhara kwa wananchi na mali zao ikwemo majeruhi, vifo, uharibifu wa mazao, miundombinu na vifo vya mifugo.’’ alisema Dkt. Lobora.
Amesisitiza kuwa kwa sasa Wizara imekuja na mkakati wa matumizi ya teknolojia kuhakikisha inapata taarifa sahihi na kwa haraka kupitia mfumo wa kidijitali ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu ulipaji wa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wakati.
Awali, Bi. Kay Kagaruki, Mkurugenzi Msaidizi Matumizi ya Wanyamapori kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori alisema kuwa, juhudi za Serikali katika uhifadhi wa rasilimali za maliasili wakiwemo wanyamapori zinaungwa mkono na wadau mbalimbali hata hivyo hivyo, amesisitiza kuwa uhifadhi wa wanyamapori bado unakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo migongano baina ya binadamu na wanyamapori, ujangili wa wanyamapori.
“Katika kuimarisha utatuzi wa changamoto hizo, Wizara imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa Mfumo wa kielektroniki wa kukusanya na kuchakata taarifa ya matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu uwandani (Problem Animals Information System-PAIS) ili kuharakisha utoaji wa taarifa hizo kwa ajili ya udhibiti na ulipaji wa kifuta jasho na kifuta machozi kwa wakati. “alisema Bi. Kagaruki.
Naye Bw. Theodory Mulokozi, Afisa Mazingira Mwandamizi OR- TAMISEMI, aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa mafunzo hayo na kutoa vitendea kazi kwa ajili ya ukusanyaji wa taarifa husika na kutoa wito kwa Maafisa Ugani kutumia vitendea kazi walivyokabidhiwa kwa kazi iliyokusudiwa na si vinginevyo.