Mwamvua Mwinyi, Pwani
Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), imekuja na mikakati mipya ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kukuza ushindani na maendeleo ya sekta ya uwekezaji nchini.
Kupitia kongani ya kibiashara ya Kwala, iliyopo Kibaha mkoani Pwani, TISEZA inatoa fursa mbalimbali kwa wawekezaji, ikiwemo utoaji wa maeneo bure kwa wawekezaji watakaokamilisha ujenzi wa miradi yao ndani ya kipindi cha miezi 12.
Kaimu Ofisa Mawasiliano wa Umma wa TISEZA, Adelina Rushekia, alieleza hayo wakati wa ziara ya waandishi wa habari katika eneo la Kwala, Septemba 30, 2025.
Alisema kongani hiyo yenye ukubwa wa hekta 100 ni miongoni mwa miradi inayotangazwa kwa sasa na mamlaka hiyo.
Kwa mujibu wa Adelina, wawekezaji wa ndani wanaruhusiwa kuwekeza kwa mtaji wa kuanzia Dola za Kimarekani milioni 5 (sawa na takriban sh. bilioni 12.5), huku wawekezaji wa nje wakitakiwa kuwa na mtaji wa kuanzia Dola milioni 10 (sawa na sh. bilioni 25).
“Tunawahamasisha wawekezaji kukimbilia kuwekeza kwa kuwa kuna fursa nyingi na kuunganishwa na taasisi wezeshi kama NEMC na OSHA,” alisema.
Alitaja maeneo mengine yanayotangazwa na TISEZA kwa ajili ya uwekezaji kuwa ni pamoja na Buzwagi mahususi kwa ajili ya uchenjuaji wa madini na Nala, Dodoma.
“Hii ni hatua mpya ya TISEZA kuinua na kukuza sekta ya uwekezaji mkoani Pwani na Tanzania kwa ujumla,” alisisitiza Adelina.
Kwa sasa, Adelina alieleza kuwa tayari wawekezaji 10 ambao wengi wao ni wazawa wameonyesha nia ya kuwekeza katika kongani ya Kwala.
Kwa upande wake, Gerald Tiria, msimamizi wa kiwanda cha kuzalisha majokofu kilichopo katika kongani hiyo, alieleza kiwanda hicho kimeajiri vijana 30 wa Kitanzania, ambapo 25 kati yao wana mikataba ya ajira rasmi.
“Vijana wetu wana uwezo mkubwa wa kutengeneza bidhaa hizi, awali tulifundishwa na wachina sita ambao tayari wamesharejea kwao, na sasa amebaki mmoja anayehusika na masuala ya ofisini,” alieleza Tiria.
Kiwanda hicho huzalisha majokofu madogo kati ya 100 hadi 130 kwa siku, pamoja na majokofu makubwa 10 kwa siku.