NA DENIS MLOWE, MAFINGA
RAFIKI Australia kwa kushirikiana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Cosato Chumi pamoja na Wizara ya Afya (MOH), wamezindua mpango wa kuwagawia Taulo za kike wanafunzi wa shule za Sekondari na Msingi katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga.
Msaada huo wa Taulo za Kike 500 umezinufaisha wasichana wa Shule ya Sekondari Kinyanambo na Shule ya Msingi Mkombwe zilizoko Mafinga.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, Afisa mradi , Saum Zidadu alisema kuwa hatua ya Rafiki kuanzisha kampeni ya Rafiki wa Binti ni sehemu ya kuunga mkono jitihada za kumpatia mtoto wa kike hedhi salama.
Alisema kuwa wanataka kuhakikisha msichana wa Kitanzania anabaki shuleni, anaendelea kusoma na kufikia ndoto zake bila kuzuiliwa na hedhi,.
Alisema tofauti na taulo za kibiashara zinazotumika mara moja na kutupwa, taulo hizi za kisasa zinazoletwa na Rafiki zinaweza kuoshwa na kutumika tena hiyo yote ni katika kuunga mkono jitihada za serikali kupitia Wizara ya Afya, na kwa hamasa ya Cosato Chumi,.
Aliongeza kuwa Rafiki imeanzisha Rafiki wa Binti kwa lengo la kuwasaidia wasichana wa Kitanzania kupata huduma hii ya taulo za afya kwa nia ya kulinda afya zao, kuokoa muda ambao unapotea na hivyo kuwezesha kufikia malengo yao.
Ifahamike kuwa Wizara ya Afya ilizindua Mwongozo wa Kitaifa wa Afya na Usafi wa Hedhi wa mwaka 2025 ili kuwawezesha wasichana kusimamia hedhi zao kwa heshima. Mwongozo huu unaonyesha kuwa wasichana wengi nchini Tanzania hukosa hadi 25% ya siku za masomo kwa sababu ya kushindwa kudhibiti hedhi zao. Wengi wao pia wanakosa maarifa sahihi kuhusu afya na usafi wa hedhi.
“Rafiki wa Binti imejitolea kusaidia Halmashauri ya Mafinga. Hii inaanza leo kwa kugawa ‘Binti Packs’ 500, kila moja ikiwa na taulo sita za kike zinazoweza kutumika tena, kitabu cha elimu, na begi la kuhifadhia” Alisema.
Alisema kuwa Msaada huo umetolewa bure kabisa kwa wasichana wa shule, pamoja na elimu ya kubalehe na hedhi, vipimo sahihi vya taulo za kike ,maelekezo ya usafi, matumizi na namna ya kuosha.
Taulo za kike zimekuwa zikitumika kibiashara kwa zaidi ya muongo mmoja. Inakadiriwa kuwa duniani kote, zaidi ya milioni 15 za taulo hizi huuzwa kila mwaka. Huko Australia, takribani robo ya wasichana wanatumia taulo za kike za na umaarufu wake unaongezeka haraka.
Taulo hizi ni za kiubunifu kwa uwezo mkubwa wa kufyonza, salama kutumia na rafiki wa mazingira. Zikitunzwa vizuri, zinaweza kutumika tena kwa miaka miwili.
Rafiki wa Binti itaingia kwenye ushirikiano na wadau na shule ili kurahisisha ugawaji wa Binti Packs pamoja na elimu ya hedhi. Rafiki imejikita katika kuhakikisha msaada huu ni endelevu na kufanikisha upanuzi wa mradi huu ndani ya Halmashauri ya Mji Mafinga na maeneo mengine ya Tanzania.