Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Wananchi wa Kata ya Mkomazi wilayani Korogwe Mkoani Tanga wamepatiwa elimu ya kujikinga na tembo pindi wawaonapo wanyama hao kwenye makazi na mashamba yao ili kunusuru athari ambazo zinaweza kusababishwa na wanyama hao.
Aidha wananchi hao pamoja na kuishukuru serikali kwa jitihada hizo pia wameiomba serikali kuendelea kuongeza nguvu zaidi ya kuwaondoa wanyama hao kwenye makazi na mashamba yao ili kunusuru usalama wa afya na mali zao kwani wanyama hao wameendelea kuwa tishio zaidi.
Wakizungumza kwenye mafunzo ya namna ya kujikinga na tembo yaliyotolewa na askari wa uhifadhi Kutoka hifadhi ya Taifa mkomazi wananchi hao akiwemo Twalibu Iddi na Sakina Mkomwa wakazi wa Kata ya Mkomazi wilayani Korogwe Mkoani Tanga wamesema tembo wameendelea kuwa tishio kwenye maeneo hayo kwakuharibu mazao mbalimbali ya wananchi na kusababisha hasara kubwa kwa wakulima.
Wananchi hao wameiomba serikali kuona namna ya kuongeza thamani ya kifuta jasho kwani kwasasa kifuta jasho kinachotolewa pindi wanyama hao wanapofanya uharibufu kwenye mazao yao hakilingani na thamani ya gharama walizotumia.
“Kwanza tunaishukuru sana serikali yetu kwakuendelea kuona umuhimu wetu kama wananchi wa maeneo haya kwakutupatia elimu kama hii lakini pia kutujengea kituo cha askari wa uhifadhi hapa Goha hii imesaidia sana kuwafukuza tembo kwa haraka pindi wanapovamia maeneo ya mashamba yetu lakini pili tunaomba serikali kuongeza thamani ya kifuta jasho na kitolewe kwa wakati ili kumtiamoyo mkulima anapopatwa na changamoto ya tembo”.”Walisema wananchi hao”.
Wakizungumza kwenye mafunzo hayo mhifadhi daraja la kwanza Tumain Hoza Kutoka hifadhi ya Taifa mkomazi na afisa mhifadhi Mkuu Emmanuel Sisya wamesema wameendelea kutoa elimu kwa wananchi dhidi ya wanyama hao ili wananchi waweza kuchukua tahadhari pindi wawaonapo huku wakikiri ongezeko la changamoto ya tembo kwenye makazi ya wananchi na namna ambavyo wameendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuwarudisha wanyama hao hifadhini.
Hata hivyo serikali kupitia wizara ya maliasili na utalii Nchini imetoa vifaa mbalimbali kwaajili ya kufukuzia tembo kwenye makazi ya wananchi waishio kandokando ya hifadhi ya Taifa mkomazi ili kuongeza ufanisi zaidi kwa askari wa uhifadhi katika kufukuza tembo kwenye makazi ya wananchi.