Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAKATOLIKI wa machimbo ya madini ya Tanzanite, Mji mdogo wa Mirerani, Wilayani Simanjiro, Mkoani Manyara, wamefanya ibada ya misa takatifu kwenye kumbukumbu wa somo wa kigango cha Watakatifu Malaika wakuu Michael, Gabriel na Raphael, katika machimbo hayo.
Paroko msaidizi wa Parokia ya Bikira Maria Malkia wa Rozali Takatifu, Krisantus Assenga ameongoza misa hiyo kwa kuwaasa waamini na jamii kwa ujumla kila mmoja kuwajibika katika katika nafasi yake.
Wakili Paroko Assenga ameeleza kwamba kila mmoja anapaswa kujiuliza anawajibika vipi katika nafasi yake.
“Tupo hapa kuadhimisha somo wa kigango cha Watakatifu Malaika wakuu Michael, Gabriel na Raphael, tuendelee kujiuliza je tunawajibika katika nafasi zetu au tunataka tuhudumiwe?” amehoji Padri Assenga.
Amewaasa kuwa Mungu amewapa tija kubwa hivyo wawe waaminifu kwa Mungu na wasienende kinyume na Mungu katika shughuli zao za kila siku.
Pia, ameaasa wachimbaji madini kuchukua tahadhari pindi wanapokuwa wanafanya shughuli zao ili kuepuka ugonjwa wa silikosesi unaoathiri mapafu kutokana na vumbi.
Amesema wachimbaji wa madini ya Tanzanite wakati wakiendelea kumtegemea Mungu awalinde katika kazi zao, pia wanapaswa kujilinda afya zao katika kuepuka maradhi mbalimbali ikiwemo silikosesi.
“Ni kweli Mungu anatulinda katika maisha yetu ya kila siku ila sisi wenyewe tunapaswa kuchukua tahadhari za kiafya katika kuteketeza majukumu yetu ya kila siku,” amesema padri Assenga.
Mwenyekiti wa ujenzi wa kanisa la kigango hicho, Bazili Raphael ameeleza kwamba mbali na kufanyika kwa Misa ya somo wao pia waliendesha harambee ndogo ya kukamilisha ujenzi.
Bazili amesema katika harambee ndogo ya kukamilisha ujenzi wa kanisa walifanikiwa kupata fedha taslimu Shilingi 447,000 na ahadi shingi 300,000.
Amesema pia wamepatiwa ahadi ya mifuko 167 ya saruji, lori mbili za mchanga na magari matatu ya maji ya kujengea.
Katekista wa kigango hicho Martin Mbuya ameeleza kwamba kigango hicho kilianzishwa mwaka 1995 kama jumuiya.
Mbuya amesema uwepo wa kigango hicho umevutia wachimbaji wengi kuingia katika ukristo kwa kupatiwa mafundisho na kupata sakramenti mbalimbali.
“Tunamshukuru Mungu kwa kuadhimisha misa ya somo wetu huku migodini kwani kumekuwa na dhana pofotu kwamba uchimbaji unaendana na ushirikina jambo ambalo siyo kweli,” amesema Mbuya.