
Watoto watatu wamefariki dunia baada ya nyumba ya ghorofa moja kuteketea kwa moto katika Mtaa wa Kitende, Kwa Mfipa, Wilaya ya Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 10:00 alasiri katika nyumba inayomilikiwa na Marey John Balele ambapo moto huo ulianza katika sehemu ya juu ya nyumba na kusababisha vifo vya watoto hao waliokuwa wakiishi na bibi yao.
Mashuhuda wamesema kabla ya moto huo kuanza, ulisikika mlipuko mkubwa kisha sauti za watoto zikisikika wakimuita bibi yao na kueleza kuwa kuna moto. Baada ya muda mfupi, ghorofa ya juu ya nyumba hiyo ilishika moto kwa haraka na kuwapoteza watoto watatu waliotambulika kwa majina:
1. Adriela Peter Siprian (4)
2. Gracious Kadinas (3)
3. Gabriela Kadinas (1)
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limesema linafanya uchunguzi kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji ili kubaini chanzo cha moto huo. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa uchunguzi wa kitabibu.
Aidha, Jeshi la Polisi limewaasa wazazi na walezi kuhakikisha usalama wa watoto muda wote na kuchukua tahadhari dhidi ya majanga ya moto. Wananchi pia wametakiwa kutoa taarifa mapema kwa mamlaka husika pindi wanapobaini dalili za hitilafu za moto au umeme ili hatua zichukuliwe haraka na kuepusha madhara makubwa.
Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.
Â