Singida
Mgombea urais kupitia Chama cha NLD, Mhe. Hassan Doyo, akiwa katika mkutano wa kampeni mkoani Singida, amahidi kuwa endapo wananchi watampa ridhaa ya kuongoza taifa, ataunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Amesema serikali hiyo itakuwa msingi wa kuimarisha umoja, mshikamano na maridhiano ya kitaifa, sambamba na kujenga taifa linaloongozwa kwa uadilifu, uwazi na usawa.
Mhe. Doyo amebainisha kuwa kupitia Serikali ya Umoja wa Kitaifa, NLD itaweza kutoa fursa kwa watu kutoka makundi na vyama mbalimbali kushiriki moja kwa moja katika uongozi wa nchi, jambo litakalowezesha mawazo mapya na ubunifu katika kuliongoza taifa.
“Tunataka Tanzania yenye mshikamano katika jamii. Serikali ya Umoja wa Kitaifa itawaunganisha Watanzania wote bila kujali chama, kabila au dini kwa lengo la kuleta maendeleo ya pamoja. Nchi hii ni yetu sote, na kila mmoja anapaswa kushiriki kulijenga taifa letu katka dhana ya kuleta maendeleo,” alisema Mhe. Doyo.
Kwa mujibu wa kauli yake, serikali hiyo itakuwa chachu ya kusikiliza sauti za wananchi wote, kuondoa mpasuko wa kisiasa, na kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika kwa manufaa ya wote bila upendeleo.
Aidha, Mhe. Doyo ameeleza kuwa faida za Serikali ya Umoja wa Kitaifa zitahusisha kujenga mshikamano wa kitaifa ambapo kila Mtanzania atajiona sehemu ya serikali yake, kupunguza migawanyiko ya kisiasa na kijamii kwa kushirikisha vyama vyote na makundi mbalimbali, pamoja na kuwapa wananchi uwakilishi mpana ili changamoto na mawazo yao yasikike. Pia amesema serikali hiyo itaimarisha amani na mshikikamo wa kitaifa, na kuhakikisha usawa katika mgawanyo wa rasilimali ili kila mkoa na kila mwananchi anufaike na matunda ya taifa.
Mhe. Doyo amesisitiza kuwa chama chake, NLD, kimejengwa katika misingi ya ushirikiano na mshikamano wa kitaifa, na ndicho kipaumbele atakachokileta serikalini mara tu baada ya kushinda uchaguzi mkuu Oktoba 29.
Katika mwendelezo wa mikutano ya kampeni, Chama cha NLD kinatarajiwa kuelekea mkoa wa Kondoa, Iringa na Njombe.