Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Manyara
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Ilani ya uchaguzi ya CCM kifungu cha 2 (3) kinaelekeza Serikali itakayoundwa na Chama hicho iboreshe maisha ya watu na ustawi wa jamii.
Akizumgumza leo Oktoba 4,2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika Stendi ya zamani Wilaya ya Babati mkoani Manyara ambapo malfu ya wananchi wamehudhuria Dk.Samia ameeleza kifungu hicho kinaielekeza serikali kufanyakazi kwa kasi zaidi katika sekta za maendeleo ya jamii.
“Nataka niwahakikishie wale wote ambao umeme haujafika, huduma za afya hazijafika, shule zipo mbali, maji hayajafika kote tunakwenda kufikisha maendeleo hayo kwa kasi zaidi,” amesema.
Akifafanua zaidi amesema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita Serikali imetoa zaidi ya Sh.bilioni 700 katika mkoa huo kugharamia shughuli za maendeleo nje ya fedha zilizotolewa kwa miradi ya kitaifa.
Amesema kuwa kawaida kwa maendeleo yanapopatikana kuleta mahitaji mengine katika maeneo na ndiyo maana wananchi wanahitaji makubwa zaidi.
“Hayo ndiyo yaliyotufanya tuje tusimame kuomba kura kwenu mtuchague ili tukafanye yale mazuri zaidi yaliyoombwa na wagombea lakini yaliyoombwa na wazee pamoja na viongozi wa kimila wa mkoa,” amesema Dk.Samia huku akishangiliwa na wananchi.
Pamoja na hayo amesema kuwa miongoni mwa nguzo kuu ya uchumi mkoani Manyara ni utalii kwani serikali imefanya jitihada mbalimbali kukuza utalii.
Dk.Samia amesema matokeo ya jitihada hizo, Serikali imepanga katika miaka mitano ijayo idadi ya watalii iongezeke.
Kwa sasa amesema katika mkoa huo watalii waliotembelea Hifadhi ya Tarangire na Ziwa Manyara imefikia milioni 1.6 hatua iliyoongeza fursa ya ajira na mapato.
Hata hivyo amesema kwamba Serikali itaendelea kutangaza na kuongeza vivutio ili idadi kubwa zaidi ya watalii ipatikane.
“Kitaifa mpaka tunafunga mwaka 2025 tumefanikiwa kutimiza idadi tuliyoelekezwa na Ilani ya uchaguzi. Ilani ilituelekeza tuwe na watalii milioni tano wa ndani na nje ya nchi.
Amesema kwamba: “Tumefikia milioni 5.3 sasa kwa miaka mitano ijayo kitaifa lengo tulilojiwekea ni milioni nane kwa watalii wa ndani na nje ya nchi.”
Amesema kuwa utalii unatokana na hifadhi hata hivyo anatambua uwepo wa changamoto ya mgogoro kati ya Pori la Akiba la Mkungunero na vijiji vinavyozunguka katika maeneo ya Simanjiro na Kiteto.
Ameongeza licha ya kuanishwa maeneo ya mipaka bado baadhi ya wananchi wanaendelea kuingia ndani ya hifadhi.
“Walikuwa wanafuata huduma ya maji na maeneo ya kufanyia shughuli zao. Hapa mtaona maeneo mengine wanyama wanatoka kwenye hifadhi kufuata mahitaji kwa watu.
“Lakini kule Simanjiro watu wanatoka maeneo yao wanaingia kwenye hifadhi kufuata mahitaji. Sasa uhitaji ukiwepo au mnyama au binadamu anaweza kufanya chochote,” alisisitiza.
Kwa msingi huo, alisema Wizara ya Maliasili na Utalii imeagizwa kuhakikisha vijiji vilivyopo jirani na hifadhi vinapata maji ya kutosha.-
Pia, alisema katika maeneo yanayopakana na hifadhi yamekuwa yakikabiliwa na changamoto ya uwepo wanyama wakali ambao wanavamia maeneo ya watu.
Ili kukabiliana na hali hiyo, serikali imechukua hatua kujenga vituo vya kudhibiti wanyama katika maeneo hayo.
Amebainisha kuwa vituo hivyo vitakuwa na askari wa Mamlaka ya Hifadhi Wanyamapori (TAWA) na baadhi ya vijana kutoka maeneo husika watakaopewa mafunzo kushiriki shughuli hiyo.
“Vituo hivyo tumeviwekea vifaa vya kisasa, tumeanza Tanga maeneo ya Korogwe ambako wanyama wakali kama tembo tumewavisha vifaa ambavyo wakitoka drone (ndege nyuki) zinawafuata kule walipo kuwarudisha kwenye hifadhi,” amesema Dk.Samia