

MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Gerson Msigwa ametoa ufafanuzi kuhusu taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uwanja wa Benjamin Mkapa kufungiwa kwa kipindi cha miezi sita na kubainisha kuwa taarifa hiyo ni upotoshaji.
Kupitia taarifa yake ya leo Oktoba 04, 2025 kwenye ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, Msigwa amesema uwanja huo hautafungiwa bali utapunguziwa matumizi ambapo mechi za Kimataifa tu za Klabu na Timu ya Taifa zitachezwa kwa Mkapa huku sababu kuu ikiwa ni ‘pitch’ kuharibika kutokana na mfululizo wa mechi za Ligi Kuu na Kimataifa.
“ACHENI KUPOTOSHA. Hatujatangaza kuufunga Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa miezi 6 kama baadhi ya watu wanavyopotosha. Tumekaa na TFF na pia timu za Yanga na Simba zilioomba kutumia uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya mechi za ligi na kufanya tathmini ya uharibifu wa sehemu ya kuchezea (pitch) ya uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya mechi mfululizo zilizopita za Kimataifa na za ligi.”
“Tumekubaliana kuwa Yanga na Simba watafute viwanja vingine kwa ajili ya michezo ya ligi na uwanja wa Benjamin Mkapa ubaki kwa ajili ya mechi za Kimataifa, Timu ya Taifa na Dabi mpaka hapo tutakapofanya ukarabati mkubwa wa pitch.”— amesema Msigwa