Na Karama Kenyunko Michuzi Tv
WAKATI dunia nzima ikikabiliana na ongezeko la joto linalosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, watafiti nchini Tanzania wamebaini ushahidi mpya unaoonyesha kuwa miti inaweza kuwa kinga ya moja kwa moja kwa wakulima dhidi ya athari za kiafya zinazotokana na joto kali.
Utafiti huo unaojulikana kama KISHADE (Kisiki Hai Sustainable Heat Adaptation Development), unaoongozwa na LEAD Foundation kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za kitaifa na kimataifa ikiwemo London School of Hygiene and Tropical Medicine, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Meta Meta, umeonyesha kuwa kilimo mseto (agroforestry) kinaweza kuboresha afya ya wakulima na mazingira ya kazi vijijini.
Kwa kutumia teknolojia za kisasa kama vitambuzi vinavyovaliwa (wearable sensors), watafiti walifuatilia kwa wakati halisi viwango vya joto la mwili na mapigo ya moyo ya wakulima, kisha kulinganisha kati ya wale waliokuwa na miti karibu na wale waliokuwa mashambani wazi. Pia walikusanya sampuli za damu na mkojo kuchunguza athari za kiafya zinazochochewa na joto.
Akizungumza wakati wa Jukwaa la KISHADE lililofanyika sambamba na Mkutano wa 12 wa Afya wa Tanzania (Tanzania healthy summit) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Dkt. Faranja Chiwanga, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani na Kiongozi wa Mradi, alisema:
“Lengo letu ni kubaini kama kulima mazao pamoja na miti kunaweza kuleta mabadiliko ya kweli katika afya za wakulima. Wakulima wanakabiliwa na hatari kubwa ya magonjwa yanayohusiana na joto, ikiwemo upungufu wa maji mwilini, matatizo ya figo, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo. Utafiti huu unatoa suluhisho la moja kwa moja kupitia kivuli cha miti ambacho hupunguza joto kali.”
Kwa mujibu wa watafiti, zaidi ya 70% ya nguvukazi ya taifa inajihusisha na kilimo, hivyo athari za joto kali zinaweza kuathiri afya ya watu na pia uchumi wa taifa.
Dkt. Richard Sambaiga, Mkuu wa Idara ya Sosholojia na Anthropolojia UDSM na Mratibu wa KISHADE, alisisitiza umuhimu wa kushirikisha jamii:
“Jamii zimeonyesha mwitikio chanya. Wakulima wamekubali kutumia vifaa vya kisasa vya kufuatilia afya na kutupa data sahihi. Ushirikiano huu ni ishara kwamba utafiti huu unaweza kutoa suluhisho endelevu linalokubalika kijamii.”
Kwa upande wake, Dkt. Ivan Ivanov, mtaalamu wa Afya ya Kazini kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), alisema matokeo ya Tanzania ni ya kimataifa:
“Tunapojifunza jinsi miti inavyolinda afya ya wakulima dhidi ya joto, tunapata suluhisho rahisi linaloweza kutumika duniani kote. Utafiti huu unathibitisha kwamba asili inaweza kuwa tiba bora katika enzi ya mabadiliko ya tabianchi.”
Naye mtaalamu wa hali ya hewa kutoka TMA, alisema: “Takwimu hizi zinatupa picha mpya kuhusu athari za hali ya hewa ndogo (microclimate) katika kilimo. Matokeo haya yatasaidia kupanga mikakati sahihi ya kitaifa ya kupunguza madhara ya joto kali.”
Mbali na utafiti wa kitaaluma, taasisi za kiraia pia zimechangia. Juma Mrisho kutoka Guj Foundation, inayohusika na utunzaji wa mazingira katika ukanda wa kati, alisema wamezalisha miti zaidi ya milioni 30 kwa lengo la kurekebisha hali ya hewa:
“Tunajua madhara ya joto kali kwa mwili wa binadamu, hivyo tunataka kuona namna miti inavyosaidia mashambani kupunguza athari za kiafya na upotevu wa maji mwilini. Utafiti wetu unaonyesha kuwa joto kali lina madhara makubwa kiafya, hasa kwa wakulima, hivyo tunashauri wakulima waache baadhi ya miti mashambani ili iwe kinga.”
Alfredi Kandoya, mtaalamu wa hali ya hewa kutoka TMA, aliongeza kuwa wao wamekuwa wakishirikiana na Wizara ya Afya kufuatilia viwango vya unyevu na joto kila siku:
“Kuanzia Novemba hadi Aprili huwa ni msimu wa joto kali kuliko miezi mingine. Hali hii huathiri shughuli za kilimo na uwezo wa watu kufanya kazi. Ni muhimu wakulima kutumia taarifa hizi kupanga upandaji, mavuno na hata masoko.”
Mkulima mmoja kutoka Wilaya ya Mpwapwa, Dodoma, alisema kabla ya elimu ya KISHADE walikuwa wakikabiliwa na changamoto nyingi:
“Tulipata shida ya joto kali, ukosefu wa mvua na maradhi ya mara kwa mara kama kichwa na homa kutokana na upungufu wa maji. Sasa tumepata elimu ya ‘kisiki hai’, hali imebadilika. Mazao yameongezeka na afya imeimarika.”
Kwa mujibu wa Dkt. Faraja Chiwanga, utafiti huu unasisitiza kutumia njia za asili kama kupanda miti shambani ili kulinda si tu mazao bali pia afya za wakulima:
“Tulilinganishwa wakulima wanaofanya kazi kwenye mashamba yenye miti na wasiokuwa nayo. Matokeo ya kisayansi yanaonyesha wazi kuwa miti huongeza mavuno na kulinda afya za msingi ikiwemo moyo na figo.”
Utafiti wa KISHADE unafadhiliwa na Wellcome Trust, na unatarajiwa kutoa ushahidi wa kimataifa kwa watunga sera, watoa huduma za afya, mashirika ya maendeleo na taasisi za kimataifa kuhusu nafasi ya miti katika kulinda afya ya binadamu na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
