
JAJI MKUU wa Mahakama ya Tanzania, George Masaju, ametoa wito kwa askari wa Jeshi la Polisi, mawakili na wadau wote wa mahakama kufanya kazi kwa kushirikiana, kuheshimiana na kuepuka migongano isiyo ya lazima inayoweza kudhoofisha utoaji wa haki kwa wananchi.
Akizungumza katika kikao cha pamoja cha wadau wa mahakama kilichowakutanisha mawakili, askari wa polisi na viongozi wa sekta ya sheria, Mhe. Masaju alisema kuwa ni muhimu kila upande kutambua nafasi na wajibu wa mwenzake katika mnyororo wa haki, kwani lengo kuu ni kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati na kwa usawa.
“Utoaji wa haki unahitaji heshima na maelewano. Mahakama, Polisi, na mawakili wote ni sehemu ya mfumo mmoja. Migongano ya kibinafsi au ya kiutendaji inapoibuka, ni wananchi ndio wanaoumia,” alisema Jaji Mkuu Masaju.
Ameongeza kuwa mahusiano mazuri kati ya wadau wa haki ni msingi muhimu wa kuimarisha imani ya umma kwa mahakama na vyombo vya dola, akisisitiza kuwa taswira ya haki inajengwa kupitia ushirikiano na nidhamu ya pamoja.
“Tuwahudumie wananchi kwa weledi, maadili na uwajibikaji. Tofauti za kitaaluma tusizibadili kuwa uhasama, bali tuzitumie kama nguvu ya kuboresha mfumo wa haki,” alisisitiza.
Kikao hicho kimepangwa kuwa endelevu, kikiwa na lengo la kuimarisha mawasiliano, mafunzo na uratibu wa kazi kati ya mahakama, ofisi za wanasheria, na Jeshi la Polisi, ili kuongeza ufanisi katika kushughulikia kesi na utoaji wa haki nchini.
Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.