……..
SHIRIKA la umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Ruvuma, limezindua wiki ya huduma kwa wateja ikiongozwa na Kauli Mbiu ‘Mpango umewezekana’ na kuhaidi kuboresha zaidi huduma zake kwani dhamira ya shirika hilo ni kuendelea kuwa kinara wa kutoa huduma bora zinazokidhi mahitaji kwa Watanzania.
Meneja wa Tanzania Mkoa wa Ruvuma Elius Mhelela amesema,Kauli mbiu ya Mpango umewezekana”siyo ya maneno tu bali ni ahadi wanayoitekeleza kila siku kama sehemu ya mkakati wao na utamaduni wa Tanesco kuyapa maslahi ya wateja kipaumbele.
“Kauli mbiu ya mwaka huu inaonesha kwamba suala la kutoa huduma bora kwetu sio maneno maneno,bali ni ukweli ulio dhahiri kwamba huduma bora kwa wateja ni jambo tunalolitekeleza kila siku kwa kuwafikia na kuwapa wateja wetu huduma wanazohitaji”alisema Mhelela.
Kwa mujibu wa Mhelela,wiki ya huduma kwa wateja Tanesco inatambua na kuthamini umuhimu kwa wateja wake, na wamejipanga kuhakikisha wateja wanapata huduma kwa haraka ikiwemo kuwafikishia umeme wale wote walioomba kuunganishiwa huduma hiyo.
Aidha,amewapongeza wafanyakazi,kwa kazi nzuri wanayoifanya hatua iliyowezesha shirika kupata sifa kubwa ikilinganisha na taasisi nyingine za umma katika Mkoa wa Ruvuma na kuwasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa weledi,bidii,uadilifu na uaminifu mkubwa mambo yatakayoiletea Shirika hilo sifa kubwa kwa jamii na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake mwakilishi wa Tanesco makao makuu Griffin Macha,amewapongeza wafanyakazi wa Mkoa wa Ruvuma kwa namna wanavyoshirikiana katika kutekeleza majukumu ya kuwahudumia wateja.
Alisema,kuna mambo mengi kama shirika imeyafanya ili kukamiridha dhamira ya Mpango umewezekana hasa kutoa huduma kwa wateja kupitia namba ya dharura ya 180 ambayo imerahisisha wateja kuwafikia kiurahisi zaidi nchi nzima na kupata huduma wanazohitaji.
Alisema,kuanzishwa kwa madawati ya huduma kwa wateja katika mikoa yote hapa nchini yamerahisisha Tanesco Makao makuu kupata taarifa nyingi kutoka kwa wateja wanaohitaji huduma na wale wenye changamoto hivyo kutatua kwa wakati ikilinganisha na miaka ya nyuma.
Alieleza kuwa,kituo cha huduma kwa wateja makao makuu kwa siku moja kinapokea zaidi ya simu 2,000 kati ya hizo simu 1,000 zinatoka mikoani kitu ambacho kimesaidia sana kuboresha na kuimarisha huduma,hivyo kupelekea hata taasisi nyingine Kwenda kujifunza Tanesco.
Mkuu wa kitengo cha Uhusiano na huduma kwa wateja Tanesco Mkoa wa Ruvuma Allan Njiro alisema,katika wiki ya huduma kwa wateja wafanyakazi wa shirika hilo watakwenda maeneo mbalimbali ili kutoa huduma kwa wateja wao ikiwemo kusikiliza changamoto zilizopata na kuzifanyia kazi.
“Hii ni wiki kubwa kwetu sisi kama Shirika la umma,kwa hiyo ni lazima tuhakikishe wateja wetu wanaoingia ndani na wale wa nje wanapata huduma nzuri ikiwemo majibu mazuri kulingana na changamoto za wateja wetu”alisema.
Amewasisitiza watumishi,kuhakikisha wanaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wanaofika kwenye idara zao kwa kuwa dhamira ya Shirika hilo kuendelea kuwa kinara wa kutoa huduma kwa jamii.