……..
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke limezindua Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kuandaa mdahalo uliowakutanisha Wafanyakazi na Wakuu wa Idara kujadili mafanikio na mikakati ya utoaji huduma bora na kwa wakati.
Katika uzinduzi huo Wafanyakazi wa TANESCO Mkoa wa Temeke kwa kushiriki na Wakuu wa Idara walijadili mipango iliyowezekana na kuweka mikakati ijayo, kupata uelewa wa pamoja kuhusu wiki ya huduma kwa wateja, kupitia makala inayoonesha mipango iliyotekelezwa katika mkoa huo.
Akizungumza leo Oktoba 6, 2025 wakati akizindua wiki ya huduma kwa Wateja uliofanyika Ofisi za TANESCO Mkoa wa Temeke, Kurasini, Dar es Salaam, Meneja wa wa Mkoa huo, Mhandisi Ezekiel Mashola, amesema kuwa Shirika limepiga hatua kubwa katika kutoa huduma bora kwa haraka ambapo awali mteja aliunganishiwa umeme ndani ya siku 60, lakini sasa huduma hiyo inatolewa ndani ya siku 14.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Temeke, Lucia Renatus, aliwaeleza wafanyakazi kuhusu kauli mbiu ya Mpango umewezekana katika kuhudumia wateja na kuwakumbusha kuwa mteja hatakumbuka huduma uliyompatia bali atakumbuka ulivyomfanya ajisikie wakati unampatia huduma.
Maadhimisho hayo yameanza rasmi leo, Jumatatu Oktoba 6, 2025, na yanatarajiwa kufungwa Ijumaa Oktoba 11, 2025, yakihusisha ziara kwa wateja, utoaji wa huduma mbalimbali na zawadi, pamoja na kushiriki shughuli za kijamii.
Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kila mwaka duniani kote katika wiki ya kwanza ya Oktoba, ikiwa ni fursa kwa taasisi na mashirika kuonesha kuthamini mchango wa wateja kupitia utoaji wa huduma bora, kupokea maoni na kutatua changamoto.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu ni: “Mapango Umewezekana.”