Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Mwanza
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan anatarajia kuanza mikutano ya kampeni leo Oktoba 7 ,2025 katika mkoa wa Mwanza na kisha ataendelea na mikoa mingine ya kanda ya ziwa.
Wakati Dk.Samia akitarajia kuanza mikutano ya kanda ya ziwa leo Oktoba 7,2025 tayari ameshafanya mikutano 77, katika mikoa 21, kwenye kanda za Kati, Magharibi, Pwani, Kusini, Nyanda za Juu Kusini, Pemba na Unguja (Zanzibar), vilevile Kanda ya Kaskazini.
Katika mikutano yake zaidi ya watu milioni 14.62 wamejitokeza kwenye mikutano moja kwa moja na watu milioni 31.6, wamefuatilia kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.Mikutano yote hiyo, kanda kwa kanda, mkoa hadi mkoa, mahudhurio yamekuwa makubwa.
Kwa mujibu wa ratiba ya mikutano ya kampeni ya mgombea urais Dk.Samia baada ya kumaliza katika kanda hizo leo Oktoba 7,2025 ndio anaanza na mikoa ya Kanda ya Ziwa yenye mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita, Mara na Kagera.
Na leo Oktoba 7,mwaka 2025 ataanza katikawilaya za Misungwi na Sengerema katika Mkoa wa Mwanza na Oktoba 8 mwaka huu atafanya mkutano mkubwa kampeni.
Hata hivyo matarajio ni kwamba mikutano ya mgombea urais wetu itaendelea
kufanya vizuri kwa sababu ya mafanikio yaliyopatikana kwenye kanda hiyo chini ya ongozi wake.
Miongoni kwa miradi iliyotekelezwa na kukamilika ni Daraja la Busisi (Daraja la Magufuli), kukamilika kwa ujenzi wa chanzo cha maji acha Butimba, kinachowanufaisha wananchi 450,000 Mwanza.
Pia kufanikiwa kwa mradi wa maji ya Ziwa Victoria, unawahudumia wananchi 86,980 wa Tinde na Shelui. Ujenzi wa vivuko sita Ziwa Victoria vimekamilika na kuanza kazi.
Aidha boti ya kuhudumia majeruhi wa ajali (Ambulance), Ziwa Victoria. Chanjo ya mifugo imezinduliwa na Shilingi bilioni 62 imetolewa.
Hayo na mengine yaliyofanyika, Dkt Samia bado ana fungu la neema kwa watu wa Kanda ya Ziwa. Hivyo ni muhimu wajitokeze kwa wingi kumsiiliza kuanzia Oktoba 7, 2025, Misungwi, Usagara na Sengerema.
Katibu wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo kutoka Chama Cha Mapinduzi(CCM) wakati jana anaelezea Mgombea urais Dk.Samia kwamba anaanza ziara mikoa ya Kanda ya Ziwa ,Kenani Kihongosi aliwaambia waandishi wa habari kuwa Dk.Samia ameendelea kufanya kampeni za kistaarabu, zinazozingatia utu wa Mtanzania.
Hivyo alitoa mwito zaidi ni kwa kila Mtanzania kuwa mlinzi wa amani ya nchi, kwani amani na utulivu ndiyo tunu yetu Watanzania.“Kipindi hiki cha lala salama, CCM tumejipanga
kikamilifu kuhakikisha tunamfikia kila Mtanzania na kumhamasisha akapige kura.
“Tumejipanga pia kupata ushindi wa kishindo kwa mgombea wetu wa urais wabunge na madiwani,”amesema Kihongosi alipokuwa akielezea ziara ya kampeni ya Dk.Samia kuanzia Oktoba 7,2025.