
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imefanya marekebisho ya takwimu za wapiga kura na vituo vya kupigia kura vitakavyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, baada ya kupokea taarifa rasmi kutoka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo, Oktoba 7, 2025, na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa INEC, Ramadhan Kailima, hatua hiyo imefuata baada ya kukamilika kwa uchakataji wa taarifa za wapiga kura waliopo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura la Zanzibar.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa jumla ya wapiga kura walioandikishwa ni 37,647,235, ikilinganishwa na 37,655,559 waliotangazwa awali. Kati ya idadi hiyo, 36,650,932 ni wapiga kura wa Tanzania Bara na 996,303 ni wa Tanzania Zanzibar.
Aidha, taarifa hiyo imeonesha kuwa asilimia 50.34 ya wapiga kura wote ni wanawake, huku asilimia 49.66 wakiwa wanaume.
Kuhusu vituo vya kupigia kura, INEC imeeleza kuwa vitakuwa jumla ya 99,895, kati ya hivyo 97,348 vitakuwa Tanzania Bara na 2,547 vitakuwa Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Zanzibar pekee ina wapiga kura 717,557 watakaopiga kura katika vituo 1,752, kufuatia mabadiliko yaliyowasilishwa na ZEC tarehe 26 Julai 2025.
INEC imeongeza kuwa idadi hiyo ya vituo na wapiga kura itakabidhiwa rasmi kwa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ili kuwezesha maandalizi ya uangalizi na usimamizi wa uchaguzi kwa mujibu wa sheria.