*Kiongozi wa Mbio za Mwenge kitaifa Asema Sekta ya Madini Inafanya Vizur
*Kimegharimu Shilingi Bilioni 2, kinamilikiwa na Kampuni ya Ken Gold
*Mkuu wa Wilaya Asema Chunya Haivumi kwa Madini lakini Imo
Chunya
Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka 2025 Ismail Ussi amezindua Kiwanda cha Kuchenjua Madini ya Dhahabu Wilayani Chunya cha Kampuni ya Ken Gold kilichogharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 2.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Oktoba 7, 2025, Ussi amesema Mbeya ni Mkoa unaendelea kufanya vizuri katika Sekta ya Madini hususan Wilaya ya Chunya kutokana na shughuli za madini na kuongeza kwamba, Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wazawa na wageni.
Ameeleza kuwa, moja ya masuala ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akiyapa msukumo ni Sekta ya Madini na hususan ushiriki wa wazawa kwenye uchumi wa madini.
“Mhe. Mkuu wa Wilaya tuwape ushirikiano wa kutosha wawekezaji wetu wakiwemo wazawa. Mfano mwekezaji huyu mzawa angeweza kwenda kuwekeza mkoa mwingine wenye madini lakini amechagua Chunya. Mwenge wa Uhuru umewaka Sekta ya Madini na kutoa heshima,” amesema Ussi.
Awali, Mkuu wa Wilaya ya Chunya Mhe Mbarak Alhaji Batenga amesema hadi sasa Wilaya hiyo ina jumla ya mitambo ya kuchenjua dhahabu ipatayo 45 na kwamba ni mkoa wa pili wa kimadini kwa uzalishaji wa dhahabu baada ya Geita.
” Ndugu Kiongozi wa Mwenge, Mhe. Dkt. Samia Suluhu ametupa maelekezo ya kulinda rasilimali zetu, na nikueleze tu Chunya ni Wilaya isiyovuma kwenye madini lakini ipo. Sisi ni wa pili kwa uzalishaji wa dhahabu nyuma ya Geita,’’ amesema Batenga.
Ameongeza kwamba, shughuli za uchimbaji madini zinaendelea kuchangia maendeleo na kutolea mfano wa uchimbaji mdogo kwamba hivi sasa mchango wa wachimbaji wadogo kwenye maduhuli ya Serikali umefikia asilimia 40.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum na timu ya Madini Diary, Mkurugenzi wa Kampuni ya Ken Gold ambaye ndiye mmiliki wa kiwanda hicho cha kuchenjua dhahabu
Kenneth Mwakyusa amesema mara tu baada ya uzinduzi, kiwanda hicho kitaanza uzalishaji wa dhahabu kutumia mitungi minane iliyopo sasa yenye uwezo wa kila mmoja kubeba tani 5. Mbali ya kumiliki kiwanda hicho, Mwakyusa pia ni mchimbaji, mnunuzi na mfanya biashara wa madini ya dhahabu na mmiliki wa timu ya mpira ya Ken Gold Sports Club ya Chunya.
Amesema upo mpango wa kuongeza mitambo mingine ya uzalishaji kwani tayari miundombinu kwa ajili ya kusimika mitambo mingine imekwishaandaliwa na kuongeza kwamba, mitambo ya kiwanda hicho ipo inayotumia mvuke badala ya maji.
Mwakyusa ameipongeza Serikali kwa kuboresha mazingira ya uchimbaji na biashara ya Madini kwani sasa shughuli hizo zinafanyika vizuri na kuendelea kuchochea maelfu ya watanzania kuingia kwenye mnyororo wa shughuli za madini.
“Mimi nimefika hapa kwa sababu ya madini nimeanza shughuli hizi kwa miaka mingi, mbali na uuzaji na uchimbaji wa dhahabu ninamiliki shule ya msingi ya english medium hapa Chunya ikiwemo timu ya mpira wa miguu ya Ken gold na miradi mengine. Nimeajiri watanzania na fedha zote nimepata kwenye madini kwa hiyo ni kweli madini ni maisha na utajiri. Kinachotakiwa ni uvumilivu na kufuata matakwa ya Sheria” amesisitiza Mwakyusa.
Ameongeza kwamba mitambo kama hiyo inawasaidia kuwaondoa wachimbaji kwenye matumizi ya zebaki kwasababu hiyo haitumii zebaki na hivyo kuongeza usalama na afya za wachimbaji na wachenjuaji.
Awali, akitoa taarifa kwa kiongozi wa mwenge, Kaimu Mkurugenzi wa Ken Gold Nelson Mpocha amesema kiwanda hicho kinatarajia kutoa ajira kwa watu 60 na tayari 15 kati yao wana ajira. Ameyataja manufaa ya kiwanda hicho ni pamoja na mapato kwa serikali, ajira na kuwasaidia wachimbaji wadogo shughuli za kuchenjua kupitia mitambo huo wa kisasa.