Na Mwandishi Wetu, Barcelona – Hispania
Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) wameendeleza jitihada za kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia ushiriki wao katika maonesho ya utalii (Tourism Road Show) yanayofanyika nchini Hispania.
Onesho hilo lililoandaliwa na kampuni ya usimamizi wa safari (DMC) yenye makao makuu yake nchini Tanzania, (Tanganyika Expeditors) na kufanyika jijini Barecelona Oktoba 06, 2025 , limewaleta pamoja wadau mbalimbali wa sekta ya utalii wakiwemo mawakala wa safari za kitalii pamoja na wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya jiji hilo.
Kupitia ushiriki huo, NGORONGORO na TANAPA zimepata fursa kutoa taarifa muhimu za kuwasaidia mawakala wa usafiri kuandaa safari kwa wageni wanaotaka kutembelea Tanzania kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana hifadhi ya Ngorongoro na Hifadhi za taifa kama vile Serengeti, Manyara, Tarangire na maeneo mengine ya kipekee yanayosimamiwa na taasisi hizo.
Mbali na NCAA na TANAPA, washiriki wengine kutoka Tanzania ni pamoja na Miracle Experience -Tanzania, Auram Treks, Karafuu Beach Resort and Spa na Malia Hotels International.
Maonesho hayo ya Tourism Road Show yaliyoanza leo tarehe 6 Oktoba yataendelea kufanyika katika majiji mengine ya Hispania, ikiwemo Madrid na Seville ambapo yanatajiwa kuhitimishwa tarehe 8 Oktoba, 2025.