Afisa Mahusiano wa TANESCO Angelina Bidya wakati akizungumza mara baada ya kukabidhi jiko la umeme linalotumia nishati kidogo kwa familia ya Safari.
Wa kwanza kushoto ni Bw. Safari na familia yake wakati akikabidhiwa jiko la umeme linalotumia nishati kidogo
Salome Safari akizungumza kwa niaba ya familia ya Bw.Safari mara baada ya kuwekewa umeme na kukabidhiwa jiko la umeme linalotumia nishati kidogo.
……………..
Na Neema Mtuka Sumbawanga
Rukwa :Shirika la Umeme Tanzania — (TANESCO), limeendelea kurejesha faraja kwa wananchi kupitia huduma zake za kijamii, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka huu 2025.
Katika mkoa wa Rukwa, shirika hilo limeunganishia umeme familia ya Bw. Safari Ally, wa kijiji cha pito manispaa ya Sumbawanga ambaye ana mahitaji maalumu kutokana na changamoto ya kuzungumza.
Mbali na hilo, (TANESCO) ,pia imemkabidhi jiko la umeme linalotumia nishati kidogo, ikiwa ni hatua ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa wananchi.
Akizungumza kwa niaba ya familia ya Safari Salome Safari amelishukuru shirika hilo kwa msaada huo ambao umewapunguzia ukali wa maisha kwani wana uwezo wa kutumia umeme kujiingizia kipato.
“Ninawashukuru TANESCO kwa msaada huu nitabuni biashara mbalimbali zitakazo niingizia kipato na nitaondokana na changamoto ya kuombaomba”amesema Salome.
Akizungumza wakati wa tukio hilo leo Oktoba 7, 2925 Afisa Mahusiano wa TANESCO Mkoa wa Rukwa, Bi. Angeline Bidya, amesema kuwa ni utamaduni wa shirika hilo kila mwaka, wakati wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, kurudisha fadhila kwa jamii kwa kutekeleza miradi midogo yenye kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja.
Bi. Bidya ameongeza kuwa TANESCO itaendelea kutoa huduma bora kwa wateja wake na kushirikiana nao katika kulinda miundombinu ya umeme kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Shirika hilo limekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja wake kwa kuwa wanatambua mchango wao ,ambapo hutumia wiki ya huduma kwa wateja kurejesha fadhila kwa wateja wao.