Ushiriki wa makundi maalumu hasa wanawake na vijana umetajwa kuwa muhimu katika kusimamia na kulinda matumbawe, kutokana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na shughuli za kibinadamu zinazoathiri mazingira ya baharini.
Imeelezwa kuwa mazalia ya samaki yanachangia kutoa kipato na kulinda uhai wa bahari, lakini changamoto za uharibifu wa mazingira ya baharini zimeendelea kuathiri wadau mbalimbali waliopo katika jamii.
Aidha, imebainika kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanywa, wanawake wengi bado hawana uelewa wa kutosha kuhusu umuhimu wa matumbawe, kutokana na ukweli kwamba mara nyingi hubaki pwani na hawashiriki moja kwa moja katika shughuli za uvuvi. Hali hii inawafanya wawe mbali na masuala yanayohusu uharibifu wa matumbawe, japokuwa wanaguswa kwa namna mbalimbali na matokeo yake.
Kutokana na hilo, imeelezwa kuwa kuna maandalizi ya programu maalumu zitakazosaidia kuongeza uelewa wa wanawake kuhusu umuhimu wa matumbawe, sambamba na kuweka mikakati endelevu itakayohakikisha bahari inaendelea kutoa faida kwa taifa zima, jamii kwa ujumla na kwao binafsi.