
Serikali ya Chad imeiondoa taasisi ya African Parks mamlaka ya kusimamia hifadhi zake za wanyamapori, ikilishutumu shirika hilo lisilo la kiserikali kwa kushindwa kudhibiti ujangili na kuonyesha “kutoheshimu” mamlaka za serikali.
Waziri wa Mazingira, Hassan Bakhit Djamous, alisema kumekuwa na ongezeko la ujangili na kupungua kwa uwekezaji katika hifadhi zinazosimamiwa na shirika hilo. Uamuzi huo unaweka kikomo ushirikiano wa miaka 15 kati ya Chad na African Parks, ambao ulijikita katika kulinda tembo na kupambana na ujangili katika Hifadhi ya Ennedi Natural and Cultural Reserve pamoja na Greater Zakouma Ecosystem.
African Parks, ambalo mmoja wa wajumbe wa bodi yake ni Prince Harry limesema linafanya mazungumzo na serikali ya Chad “ili kuelewa msimamo wake” na kujadili njia bora ya kuendelea kulinda maeneo hayo muhimu ya uhifadhi.
Shirika hilo lilianzishwa mwaka 2000 na limekuwa likisimamia hifadhi katika nchi mbalimbali za Afrika, likijulikana kwa usimamizi wa moja kwa moja na uwajibikaji mkubwa katika kulinda wanyamapori. Hata hivyo, hivi karibuni limekumbwa na lawama baada ya kukiri kuwa walinzi wake katika hifadhi moja nchini Jamhuri ya Kongo walihusishwa na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya jamii za kiasili zilizohamishwa wakati hifadhi hiyo ilipoundwa.