Arusha
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kwa kushirikiana na wataalam wa jiosayansi kutoka Chuo Kikuu cha Goethe cha nchini Ujerumani wafanya utafiti wa jiosayansi katika Mlima Oldoinyo Lengai.
Akielezea kuhusu utafiti huo, Mkurugenzi wa Huduma za Jiolojia GST, Dkt. Ronald Massawe amesema kuwa, Mlima Oldoinyo Lengai ni moja ya milima ya volkano ambayo ipo hai, lakini pia ni mlima pekee duniani ambao volkano yake inatoa lava ya aina ya “natrocarbonatite” ambapo lava hii inapokauka na kugeuka vumbi, huweza kuwa na madhara ya kiafya kwa binadamu na wanyama, hasa inapovutwa kupitia hewa.
Akifafanua kuhusu malengo ya utafiti huo, Dkt. Massawe amesema kuwa, kulingana na mfumo wa kijiolojia ndani ya mlima, utafiti huo una malengo makubwa matatu ambayo ni: kuchunguza muundo wa ndani wa volkano, kubaini maeneo ya hifadhi ya magma na njia zake, pamoja na kutambua mabadiliko ya tabaka la miamba katika Ukanda wa Ziwa Natron.
Lengo lingine ni kuongeza uwezo wa wataalamu wa ndani hapa Tanzania, ambapo itachangia kukuza uwezo wa rasilimali watu katika kufanya tafiti za jiosayansi hususan kwenye majanga asili ya jiolojia, na lengo la tatu ni kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi katika kufanya tafiti za jiosayansi.
Dkt. Massawe amefafanua kuwa, katika awamu hii, jumla ya vituo 32 vya kufuatilia mwenendo wa mitetemo ya ardhi vimesimikwa katika eneo la mlima ambapo vituo hivyo vimewekwa katika mpangilio wa mstari wenye uelekeo wa upande wa Kaskazini-Magharibi/Kusini-Mashariki kupitia kwenye kilele cha mlima huo wenye urefu wa takriban mita 2,962 kutoka usawa wa bahari.
Sambamba na uelekeo huo, vipo baadhi ya vifaa vilivyosimikwa katika maeneo ya pembezoni na kwenye ulalo wa mlima.
Dkt. Massawe amebainisha kuwa, mtandao huu wa vifaa utanakili mitetemo ya ardhi inayosababishwa na nguvu za asili za mabadiliko ya jiolojia katika Ukanda wa Bonde la Ufa, pamoja na mitetemo inayotokana na fukuto la volkano.
Kuhusu manufaa ya kufanya utafiti huu, Dkt. Massawe ameendelea kuelezea kuwa, moja ya faida katika utafiti huu ni kwamba taarifa zitakazokusanywa katika kazi hii zitaongeza maarifa mapya kuhusu mfumo wa ndani wa volkano ya Mlima Oldoinyo Lengai na hivyo kuongeza uelewa wa hatari za kijiolojia na kuimarisha uwezo wa Serikali katika kukabiliana na majanga katika ukanda wa Ziwa Natron.
Akielezea kuhusu hali ya mlipuko katika mlima huo, Dkt. Massawe amesema kuwa, kwa mara ya mwisho Mlima Oldoinyo Lengai ulilipuka kati ya Julai, 2007 hadi 2008 na ulirusha majivu yaliyosambaa hadi umbali wa kilomita kumi (10).
Madhara yaliyojitokeza wakati wa mlipuko huo ni pamoja na vifo kwa wanyama, uharibifu wa mazingira ikiwemo maeneo ya malisho ya mifugo, pamoja na watu kuwashwa macho hadi umbali wa kilomita sabini kutoka kwenye mlima huo, alifafanua Mtaalam huyo.
Kwa kipindi kirefu GST imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali zinazohusiana na majanga asili ya jiolojia ikiwemo maporomoko ya ardhi, matetemeko ya ardhi, mipasuko na mididimio ya ardhi kwa kushirikiana na taasisi za ndani na nje ya nchi.
Utafiti huo ulihusisha wataalamu mbalimbali akiwemo Dk. Ronald Massawe na Gabriel Mbogoni kutoka GST pamoja na Prof. Georg Rumpker, Dr. Ayoub Kaviani, Christoph Locker na Ms. Kamila Diaz kutoka Chuo Kikuu cha Goethe.