Na: Calvin Gwabara – Dodoma.
Waandishi wa Sheria kutoka Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD)
wamefanya ziara ya mafunzo nchini Uingereza,
ikiwa ni sehemu ya ushiriki wao katika Mkutano
wa Jumuiya ya Waandishi wa Sheria wa Jumuiya ya Madola (Commonwealth
Association of Legislative Counsel – CALC), Kanda ya Ulaya.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Divisheni ya Urekebu wa
Sheria, Utafiti na Mafunzo wa OCPD, Bi. Rehema Katuga, amesema safari
hiyo imekuwa na manufaa makubwa kwani imewapa fursa ya kuona kwa vitendo namna
wenzao wa Uingereza wanavyotekeleza majukumu yao katika nyanja ya uandishi wa
sheria kwa kutumia mifumo ya kisasa na mipango madhubuti ya mafunzo.
“Tulipata
nafasi ya kutembelea Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Uingereza
inayojulikana kama Office of Parliamentary Counsel (OPC), ambapo tulijifunza
kwa kina jinsi wanavyofanya kazi kama taasisi huru inayojitegemea lakini yenye
uhusiano wa karibu na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na hii imetupa
mwanga juu ya namna tunavyoweza kuboresha mifumo yetu nchini,” alisema
Bi. Katuga.
Aidha Katuga amesema
kupitia ziara hiyo, maafisa hao waliweza kujifunza pia kuhusu namna nchi hizo
zinavyoshughulikia masuala ya urekebu wa sheria na jinsi mifumo yao ya utunzaji
wa kumbukumbu inavyowezesha urahisi wa kupata taarifa za kisheria kwa wananchi.
“Tunarejea
nchini tukiwa na maono mapya, tumepata somo la namna tunavyoweza kuboresha Ofisi
yetu kwa kuimarisha matumizi ya teknolojia, kubuni mpango wa mafunzo endelevu
kwa waandishi wa sheria, na kuhakikisha kuwa taratibu zote za uandishi wa
sheria zinakuwa wazi, shirikishi na zenye ufanisi,”
alihitimisha Bi. Katuga.
Bi. Katuga amesema ziara hiyo ni sehemu
ya utekelezaji wa mpango mkakati wa OCPD wa kuboresha utendaji wake kupitia
mafunzo ya kimataifa, ubadilishanaji wa uzoefu, na ushirikiano wa kikanda na
kimataifa katika nyanja ya uandishi wa sheria na urekebu wa sheria imelenga
kujifunza mbinu, mifumo na teknolojia mpya za uandishi na urekebu wa sheria ili
kuboresha utendaji wa ofisi hiyo muhimu nchini Tanzania.
Nae
Bw. Alfred Nyaronga ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA katika Ofisi ya
Mwandishi Mkuu wa Sheria amesema timu hiyo pia ilitembelea Ofisi ya Taifa ya Kumbukumbu ya Nyaraka (The
National Archives) ambako walijifunza kuhusu mfumo wa kidigitali wa Lawmaker,
unaotumika katika maandalizi, marekebisho na urekebu wa sheria nchini
Uingereza.
Amesema
mfumo wa Lawmaker ni wa kipekee unawawezesha wadau wote wa uandishi wa
sheria kuanzia wizara, bunge, ofisi ya mwandishi wa sheria, hadi mpigachapa wa
serikali kufanya kazi kwa pamoja katika
jukwaa moja la kidigitali ambapo mswada unaweza kupitiwa, kurekebishwa, na
kupitishwa hatua kwa hatua ndani ya mfumo huo hadi unapokuwa sheria kamili.
Bwana Nyaronga ameongeza kuwa mfumo
huo pia hutumika katika urekebu wa
sheria (consolidation of laws) kwa kuruhusu sheria zilizofanyiwa
marekebisho kuunganishwa moja kwa moja, hivyo kumwezesha mwananchi au mdau
yeyote kupata toleo la kisasa la sheria husika mara moja na hivyo kunaongeza uwazi, ufanisi na upatikanaji wa
taarifa za kisheria kwa umma, jambo ambalo tungependa kuona linatekelezwa pia
hapa nchini.
“Kwakweli
huo ni mfumo mzuri ambao umeleta mapinduzi makubwa kwenye masuala ya uandishi
wa sheria nchini Uingereza nasi tunashawishika kuiona umuhimu wa ofisi yetu
kuanza mazungumzo nao maana wameonesha utayari wa kutujengea uwezo watu wetu kisha
tuweze kuuleta hapa nchini ili na sisi tutoke kwenye matumizi ya karatasi
tuingie kwenye mfumo huu wa uandishi wa sheria kidigital” Alisema Nyaronga.
Kwa
upande wake Bwana Bavoo Junus, ambaye ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Uhakiki
Ubora kutoka OCPD amesema kuwa pamoja na nchi za magharibi kupiga hatua kubwa
kwenye matumizi ya teknolojia katika uandishi wa sheria lakini pia wameweza
kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoletwa na matumizi ya mifumo hiyo na
kuongeza ufanisi.
Aidha
Junus amesema jambo lingine muhimu ambalo wamejifunza kwenye ziara hiyo ambalo
wanalipa kipaumbele walipoonana na Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Uingereza, anayejulikana kama First Parliamentary Counsel, pamoja na
Second Parliamentary Counsel ni mafunzo
kuhusu jinsi wanavyosimamia shughuli za uandishi wa sheria na kuwajengea uwezo
waandishi wapya kupitia mafunzo ya ndani (in-house training).
“Wenzetu wameweka utaratibu wa kuwa na mafunzo ya
ndani ili kusaidia Waandishi wachanga na wageni kwenye fani hiyo, ambapo
waandishi wa sheria wenye uzoefu (senior drafters) hupewa wajibu wa
kuwafundisha waandishi wapya kwa kipindi cha mwaka au zaidi hivyo mfumo huu wa
ushauri na mafunzo ya vitendo umekuwa na matokeo makubwa katika kukuza ujuzi na
kuimarisha ubora wa kazi, ingawa pia ni jambo ambalo OCPD imeshaanza
kulitekeleza na tunatamani liwe endelevu,” alisema Bwana Junus.
Aliongeza” Jambo lingine tulilojifunza,
wenzetu kwenye Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria wa Uingereza ofisi yao
wameigawanya katika timu nne na kila timu ina kiongozi wake na inafanya jambo
mahususi ya kuyashughulikia kwenye sekta fulani na hivyo kuwa na ushiriki wa
jumla katika eneo husika na sio mtu mmoja kuwa na taarifa fulani pake yake na
akikosekana kazi zinasimama, hii inawezesha wote kuelewa kila jambo kwa undani
na kazi kutokwama na kuongeza ufanisi na uwajibikaji kwa wote”.
Wataalamu hao kutoka Tazania walipata
fursa ya kutembelea Bunge la Uingereza,
likijumuisha House of Commons na
House of Lords, ambapo
walijifunza kuhusu utendaji wa kila chombo cha kutunga sheria, utaratibu wa
vikao, na historia ya Bunge hilo lenye asili ndefu katika demokrasia ya
kisheria.
Uzoefu huo umefungua ukurasa mpya
katika mpango wa OCPD wa kuboresha mifumo ya ndani, ikiwemo matumizi ya teknolojia
katika uandishi wa sheria, Urekebu wa sheria,Ufasili wa sheria na usimamizi wa
kumbukumbu.