

Serikali imeendelea kuleta unafuu kwa wakulima wa zao la pamba wilayani Kasulu kwa kuwapatia pembejeo muhimu kama mbegu, viuatilifu na vinyunyizi, hatua iliyochochea kilimo chenye tija na matokeo chanya.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Mhe. Kanali Isaac Mwakisu, amesema hayo leo Jumanne, Oktoba 7, 2025, katika Kata ya Asante Nyerere, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Pamba Duniani yaliyokwenda sambamba na uzinduzi wa msimu mpya wa zao hilo kwa mwaka 2025/2026.
Amesema maadhimisho hayo ni fursa muhimu kwa Serikali, wanunuzi na vyama vya msingi kujadili maendeleo ya zao hilo na kuweka mikakati ya kuliboresha zaidi.
Aidha, amewataka wananchi kutumia kipindi hiki cha kampeni kusikiliza sera za wagombea wa vyama mbalimbali ili siku ya uchaguzi, Oktoba 29, watumie haki yao ya kikatiba kuchagua viongozi wanaowataka.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Theresia Mtewele, amesema maadhimisho ya Siku ya Pamba Duniani yaliyoanzishwa mwaka 2019 yanalenga kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa zao hilo kama chanzo kikuu cha kipato kwa wakulima wadogo na wafugaji vijijini.
Mkulima wa Pamba, Joel Kingi, ameishukuru Serikali kwa juhudi zake za kuhamasisha kilimo hicho, akieleza kuwa idadi ya wakulima imeongezeka kutoka 50 hadi kufikia 1,000 kutokana na upatikanaji wa pembejeo na viuatilifu.
Awali, Mkaguzi wa Pamba wa Wilaya hiyo, Michael Kiliga, amesema wilaya inashirikiana na vyama vya ushirika (AMCOS) nane kusambaza pembejeo kwa wakulima bure, hatua inayochangia kuimarisha uzalishaji wa zao hilo.