Na Sophia Kingimali.
Afisa ustawi wa jamii kutoka ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Judith Kimaro ametoa rai kwa wamiliki wa vituo vya kulelea watoto mchana(Daycare) kuhakikisha vinaweka mazingira mazuri kwa watoto hao lakini kuhakikisha vituo hivyo vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria.
Wito huo ameutoa jijini Dar es salaam wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya wamiliki wa vituo vya kulelea watoto mchana(DAYCARE)Yaliyoandaliwa na chuo cha ufundi VETA FURAHIKA yenye lengo la kuwakumbusha wamiliki hao umuhimu wa kutunza mazingira ya vituo vyao lakini pia usajili wa vituo hivyo ili vitambulike rasmi.
Amesema vituo hivyo ni muhimu kwa ustawi wa watoto hivyo wanapaswa kutumia lugha nzuri kwa watoto lakini kujiepusha na matendo ya kikatili kwa watoto hao.
“Serikali inatambua umuhimu wa vituo vyenu kwa ustawi wa watoto mimi niwaombe kwanza msajili vituo vyenu kwa ambao bado hamjasajili lakini pia mjiunge kwenye umoja wenu wa UVIWADA ili hata fursa zinapojotokeza nuweze kuzipata”,Amesema Kimaro
Ameongeza kuwa wamiliki wa vituo hivyo wanapaswa kuhakikisha vitendo vya ukatili kwa watoto vinakomeshwa lakini wajenge uhusiano mzuri na wazazi kwani kulea kundi la watoto walio chini ya miaka 5 kunahitaji ushirikiano ili watoto hao wapate haki zao zote za msingi.
Kwa Upande wake Kaimu Mkuu wa chuo cha VETA FURAHIKA Dkt David Msuya amesema serikali inajitahidi kuhakikisha vituo hivyo vinakuwa na mazingira mazuri lakini wamiliki wake hawaonyeshi matokeo mazuri.
Amesema ili serikali iweze kuvitambua na kutoa fursa kwa vituo hivyo ni lazima vituo visajiliwe kisheria na vifanye kazi kwa weledi.
“Lengo la mafunzo haya ni kuona jinsi kujadiliana namna wanavyolea watoto,ulinzi wa watoto lakini pia uboreshaji wa vituo hivyo ili waweze hata kukopesheka lakini ni lazima wawe wamesajiliwa na vituo vinatambuliwa kisheria”,Amesema Msuya.
Nae,Katibu wa Umoja wa vituo vya kulelea watoto wadogo (UVIWADA)Hija Duge amekipongeza chuo cha VETA FURAHIKA kwa kuandaa mafunzo hayo kwani yamekuwa yanatija katika kuboresha vituo vyao huku akitoa rai kwa vituo ambavyo avijajiunga na umoja huo kujiunga ili pindi fursa zikitokea na wao washirikishwe.
Nao,baadhi ya washiriki kwenye mafunzo hayo wameiomba serikali kuweka mifumo thabiti ya kuwatambua na kuhakikisha watoto wanapelekwa kwenye vituo ambavyo vimesajiliwa kisheria.