

Watanzania wameshauriwa kupuuza propaganda chafu zinazoenezwa na baadhi ya watu wasioitakia mema nchi ya Tanzania kwa lengo la kutaka kuchafua hali ya amani na utulivu iliyopo nchini na badala yake waendelee kuiunga mkono Serikali.
Ushauri huo umetolewa jana na mjumbe wa Mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja katika hotuba yake kwenye mkutano wa kampeni za kumnadi mgombea udiwani kwa tiketi ya CCM kata ya Kilago wilayani Kahama ambao umefanyika kwenye kijiji cha Shininga.
Mgeja ambaye pia ni Mwenyekiti Mstaafu wa CCM mkoa wa Shinyanga alisema Watanzania hawapaswi kuwa na hofu yoyote kutokana na maneno ya upotoshaji dhidi ya Serikali yanayosambazwa kupitia mitandao ya kijamii na badala yake wajitokeze kwa wingi Oktoba 29, 2025 kwenda kuwachagua wagombea wanaotokana na CCM akiwemo mama yetu shupavu Rais Dkt. Samia.
Alisema watanzania wengi bado wana imani kubwa na Serikali yao inayoongozwa na mwanamke shupavu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba anaamini mikakati yote michafu yenye lengo la kumchafua itashindwa na hakuna mtanzania mwenye akili timamu atakayeunga mkono mikakati hiyo.
“Niwaombe watanzania wenzangu wenye imani na nchi yetu, tuondoe hofu na siku ya kupiga kura Oktoba 29 tujitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura kwa viongozi wanaotokana na CCM ikiwemo kumpigia kura za kishindo mgombea urais wa CCM Dkt. Samia Suluhu Hassani,”
“Mbali ya kumchagua Rais lakini pia tuwapigie kura nyingi wagombea nafasi za ubunge na udiwani wanaotokana na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama pekee chenye dhamira ya dhati ya kuwaletea watanzania maendeleo ya kweli, na tuwapuuze wale wote wenye nia ya kutaka kutuletea machafuko,” alieleza Mgeja.
Alisema Watanzania bado wana imani kubwa na vyombo vya ulinzi na usalama wakiamini vinafanya kazi zake vizuri kwa mujibu wa sheria zilizopo za nchi pamoja na kanuni zake kwa kuzingatia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mgeja ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo Foundation yenye makao yake makuu Mjini Kahama aliendelea kueleza kuwa masuala ya kulinda amani ya nchi ni endelevu na jukumu lakini kila mtanzania mpenda amani katika nchi hii bila kujali itikadi za kisiasa, kidini wala ukabila.
Aliwaomba Watanzania waendelee kuilinda amani iliyopo kwa wivu mkubwa na wasikubali wala kumkubalia mtu ye yote anayetaka kuleta uvunjifu na chokochoko katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi mkuu hapa nchini.
“Mimi narudia tena kuwaomba watanzania tuendelee kumuunga mkono Rais wetu na sote kwa umoja wetu tujitokeze kwenda kumpigia kura za kishindo Rais Samia ifikapo Oktoba 29, 2025 na tupuuze wanaosambaza kauli za “No Reform No Election,” ni kauli za kupuuzwa na kulaniwa,”
“Kila Mtanzania anapaswa kuangalia kazi kubwa zilizofanywa na Rais Dkt. Samia ndani ya kipindi cha miaka minne, kafanya makubwa, kaendeleza na kukamilisha miradi mingi iliyoasisiwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, bila ya kuitelekeza, anastahili pongezi, na pongezi hizo ni kumpa kura za kishindo,” alieleza Mgeja.
Aliendelea kufafanua kuwa kila Mtanzania anapaswa kuwa makini katika kuchambua pumba na mchele katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, kwa vile mara nyingi huzuka mambo mengi ya upotoshaji kwa lengo la kutaka kuichafua Serikali iliyopo madarakani hivyo tahadhari kubwa huhitajika.
Katika hatua nyingine Mgeja ameviomba vyombo vya dola kusimama imara katika kipindi hiki kwa kuwadhibiti kwa haraka wale wote wanaoanza kueneza habari za taharuki miongoni mwa watanzania ikiwemo wanaohamasisha makundi ya vijana kufanya vurugu zisizokuwa na msingi katika baadhi ya miji hapa nchini.
“Niviombe vyombo vyote vya ulinzi na usalama kuwa makini na kuongeza nguvu zaidi katika kipindi hiki kwa kuhakikisha wanawadhibiti na kuwachukulia hatua za haraka wale wote wenye viashiria vya kutaka kuleta vurugu na kusababisha machafuko nchini,”
“Tuwe makini sana, maana hata zile vurugu za hivi karibuni kule jijini Dar es Salaam za kushambuliwa kwa mabasi ya mwendo kasi zinapaswa kuchunguzwa kwa umakini mkubwa, ni moja ya cheche ambazo zisipodhibitiwa mapema moto unaweza kuripuka, tushituke mapema,” alieleza Mgeja.
Mgeja alishauri vyombo vyote husika vya ulinzi na usalama viwe na utaratibu wa kutoa taarifa mapema za kukanusha matukio yote yanayosambazwa kupitia mitandao ya kijamii ambayo mara nyingi yamesababisha taharuki miongoni mwa watanzania wapenda amani mfano tukio la hivi karibuni la mtu aliyejifanya Mwanajeshi.
“Hili tukio la huyu mtu anayejiita Meja Tesha kwa kweli limeshitua watu wengi, kwanza nilipongeze Jeshi letu kwa kutoa taarifa mapema ya ufafanuzi kwa watanzania, kauli yake imeleta taharuki kubwa na ni vyema taarifa za hatua zilizochukuliwa dhidi yake mpaka sasa ziwekwe wazi ili watanzania waelewe,” alieleza Mgeja.
Katika hatua nyingine Mgeja amekemea na kuwalaani vikali wale wote ambao wameanza kusambaza habari za kutaka kuvunjwa kwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambao ni muungamo wa mfano katika bara la Afrika na duniani kote na kwamba ye yote anayezusha suala la kuvunja muungano adhibitiwe mapema.