Agosti 8, 2025
Mafunzo Elekezi ya awali kwa watumishi wapya wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viwatilifu Tanzania (TPHPA) yamehitimishwa rasmi leo jijini Dar es Salaam, ikiwa ni utekelezaji wa Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 5 wa mwaka 2011, unaowataka waajiri kuwapatia watumishi mpya mafunzo elekezi ya awali ndani ya miezi mitatu baada ya kuanza kazi.
Akifunga mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu WA TPHPA, Prof. Joseph Ndunguru, amesema kuwa, kutokana na mafunzo yaliyotolewa kwa watumishi wapya, washiriki wanapaswa kuonyesha uadilifu, uwajibikaji, na weledi mkubwa katika kutekeleza majukumu yao. Alisisitiza kwamba mamlaka hiyo ni muhimu kwa usalama wa chakula na maendeleo ya nchi, hivyo wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuleta mafanikio kwa mamlaka katika kutekeleza majukumu yake na kuwahudumia wananchi.
Naye, Mkuu wa Chuo na mtendaji mkuu wa chuo cha Utumishi wa Umma, Dkt. Ernest Mabonesho, ametoa pongezi kwa uongozi wa mamlaka kwa kutekeleza wajibu wa kisheria wa kupatatia Mafunzo Elekezi ya awali watumishi wapya. Alisisitiza kuwa, mafunzo haya yatawawezesha washiriki kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi, na kwa pamoja, kuimarisha huduma zinazotolewa kwa wananchi, huku wakihakikisha usalama wa chakula na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Mafunzo haya, yaliyodumu kwa siku tatu kuanzia tarehe 5 hadi 8 Oktoba 2025, yamewaleta pamoja waajiriwa wapya 77 wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viwatilifu Tanzania (TPHPA).