Na Said Mwishehe,Michuzi TV- Mara
MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema katika uendeshaji wa nchi hakuna majaribio huku akifafanua unampa nchi yule ambaye unamwamini ataiendesha vyema na maslahi ya wananchi yatapatikana.
Akizungumza leo Oktoba 9,2025 mbele ya maelfu ya wananchi wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara Mgombea Urais Dk.Samia amesema ukiangalia kwa hapa Tanzania chama ambacho ukweli kitafanyakazi na maendeleo ya wananchi yatapatikana ni Chama Cha Mapinduzi peke yake.
“Mkiwapa wengine wanakwenda kuwafuja na wanakwenda kuwapoteza.Kwa sababu wakiingia kwanza ni kujifunza. Lakini utakapompa jimbo asiyekuwa wa CCM anakwenda kuongea na nani? Anakwenda kumuomba barabara nani?.
“Atakwenda kumuomba maji nani? Kwa sababu serikali ni ya Chama Cha Mapinduzi na yeye ni mpinzani. Ndugu zangu msicheze na hiyo kitu kabisa kabisa. Pelekeni kura kwa wateuliwa, wateuliwa hawa ni wagombea wa chama cha mapinduzi. Wapeni kura safari yetu ya maendeleo iendelee.”
Mgombea Urais Dk.Samia amewataka wananchi wasidanganyike kwani maendeleo na maslahi yao yatatokana na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi(CCM).
Kuhusu huduma mbalimbali kama maji,umeme, kilimo, barabara,afya,kilimo na huduma za jamiii Serikali imefanya kazi kubwa ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akizungumza kuhusu huduma ya upatikanaji umeme Serikali imepeleka umeme kwa kila kijiji ambapo kazi inayoendelea sasa ni kusambaza maeneo ya vitongoji.
Ameeleza kuwa katika ilani ya uchaguzi CCM ina sera za aina mbili ambapo kwanza ni maendele ya jamii yenye kujumuisha maji, umeme, afya na elimu.
Pia, amesema imani ya CCM ni kuhakikisha mwananchi anakuwa salama katika maeneo hayo hatua itakayowezesha kuchangia uchumi wa nchi.
“Tunakwenda kukamilisha kwenye maendeleo ya jamii lakini pia tunaweka nguvu katika maendeleo ya kiuchumi ambayo tunazungumzia kilimo, uvuvi, ufugaji na njia za usafiri.
“Kwa upande wa kilimo miaka mitano iliyopita tulijitahidi katika maeneo mbalimbali kujenga skimu za umwagiliaji ili wakulima walime mara mbili kwa mwaka,” amesema.
Pia amesema Serikali ilitoa mbolea na mbegu kwa ruzuku kumwezesha mkulima kuzalisha kwa wingi hatua ambayo imeleta matokeo mazuri kwa Tanzania kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 128 na kuongeza katika ilani CCM imeahidi kujenga vituo vya kilimo ambapo Mkoa wa utanufaika.
Kuhusu uvuvi amesema kwamba serikali imeanzisha vizimba 47 vya kufugia samaki pamoja na mabwawa matano katika Wilaya ya Bunda hatua ambayo imezalisha ajira kwa vijana.
“Hatutaishia hapo, ilani yetu kwa miaka mitano ijayo inazungumza tuongeze nguvu kwenye sekta ya uvuvi lakini pia tuweke viwanda vya kuchakata mazao ya uvuvi pale ambapo mazao hayo yatapatikana kwa wingi.
“Kwa kazi ambayo tumeifanya miaka mitano iliyopita tumeweza kuongeza mapato kwa wavuvi katika wilaya ya Bunda kutoka sh. bilioni tisa hadi sh. bilioni 38 fedha ambazo zimeingia mifukoni mwa wavuvi,” amesisitiza.
Kuhusu barabara Dk. Samia amesema kuwa barabara zimejengwa Nyamushwa – Bulambwa na madaraja na kuongeza nguvu katika eneo hilo kurahisisha usafiri na usafirishaji.
“Serikali inakwenda kuongeza bajeti ya barabara kwa lengo la kuzifungua katika maeneo mbalimbali nchini zipitike nyakati zote.”