NA JOHN BUKUKU- MWANZA
Mgombea wa Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema miradi mikubwa ya miundombinu inayotekelezwa jijini Mwanza itakuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na uanzishwaji wa fursa mpya za ajira, biashara na uwekezaji katika ukanda wa ziwa.
Katika sekta ya barabara, Dkt. Samia amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara ya Buhongwa–Igoma yenye urefu wa kilomita 14 kwa kiwango cha lami, huku zabuni ya ujenzi wa barabara ya Mwanza–Buhongwa–Usagara yenye njia nne na barabara ya mwendokasi ikiwa imetangazwa. Aidha, ameongeza kuwa Serikali itaendelea kujenga barabara za wilaya na mitaani ili kuunganisha makao makuu ya kata, wilaya na mikoa kwa urahisi zaidi.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo kutarahisisha usafirishaji wa bidhaa na huduma, hivyo kuongeza kasi ya shughuli za kibiashara na uwekezaji, hususan katika sekta ya viwanda na kilimo.
Dkt. Samia pia amesema Serikali itaendelea kujenga vituo vya kusambaza umeme ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa saa 24, hatua ambayo itasaidia kuongeza uzalishaji viwandani na kuboresha maisha ya wananchi. Vilevile, ametaja kuwa Serikali inaendelea kuweka kipaumbele katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya na mazingira.
Akizungumzia miradi mikubwa ya kimkakati, amesema ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) kipande cha Mwanza–Isaka chenye urefu wa kilomita 314 umefikia asilimia 63 na kugharimu Sh trilioni 3. Amebainisha kuwa stesheni tano zitakazojengwa jijini Mwanza zitakuwa fursa mpya za biashara, malazi, na huduma mbalimbali.
“Tukimaliza reli hii, safari ya Dar es Salaam hadi Mwanza itapungua kutoka saa 18 hadi saa 8 au 9 pekee, jambo litakaloongeza ufanisi wa usafiri na ushindani wa kibiashara,” amesema Dkt. Samia.
Ameongeza kuwa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia bidhaa utarahisisha biashara za ndani na nje ya nchi, huku ukiongeza ajira kwa vijana. Aidha, amesema Serikali imewekeza Sh bilioni 120.6 katika ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza iliyokamilika kwa asilimia 98, yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari 20 na malori makubwa matatu kwa wakati mmoja.
Kuhusu uwanja wa ndege wa Mwanza, Dkt. Samia ameahidi kuwa utaboreshwa kuwa wa kimataifa ili kuvutia watalii, hasa wanaoelekea Hifadhi ya Serengeti, jambo litakalopanua fursa za utalii na huduma za malazi.
Katika hatua nyingine, ameahidi kuwa Serikali itafufua viwanda vya kuzalisha vifaa tiba ikiwamo bandeji, pamba na shuka, hatua itakayopunguza uagizaji wa bidhaa hizo kutoka nje na kukuza uchumi wa ndani.
“Mwanza inakwenda kuwa kitovu cha biashara, usafiri na uwekezaji kutokana na uwepo wa miradi mikubwa ya miundombinu. Kila mradi una nafasi ya kuibua fursa mpya za maendeleo kwa wananchi wetu,” amesisitiza Dkt. Samia.