Mfanyabiashara wa chakula katika soko la Bombambili Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma Mariam Mfaume, akipika chakula kwa kutumia jiko la umeme wakati wa kampeni inayoendeshwa na Tanesco Mkoa wa Ruvuma kuhusu umuhimu wa wananchi kutumia umeme kwa kupikia.
Mfanyakazi wa kitengo cha usafirishaji Tanesco Mariam Abdul aliyeshika kipaza sauti,akitoa elimu kwa wananchi waliofika katika banda la Shirika hilo eneo la Soko la Bombambili Manispaa ya Songea kuhusu matumizi ya umeme kwa ajili ya kupikia.
…………………
Na Mwandishi Wetu, Songea.
MKUU wa kitengo cha uhusiano na huduma kwa wateja wa Shirika la Umeme Tanzania(TANESCO) Mkoani Ruvuma Allan Njiro,amewataka wananchi kutoogopa kutumia umeme kwa kupikia na matumizi mengine kwani vifaa vinavyotumia nishati hiyo hutumia umeme mdogo.
Alisema,watu wengi wamekuwa wanahofia kutumia umeme kama nishati safi ya kupikia kwa kudhani gharama ni kubwa na kubainisha kuwa,kupika chakula kama maharage kwa kutumia umeme gharama yake ni Sh.200.
Njiro amesema hayo jana,wakati akielezea faida za kutumia majiko ya umeme kwa wafanyabiashara wa soko la Bombambil lililopo kata ya Bombambili Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ikiwa sehemu ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja.
Alisema kuwa,umeme sio tu nishati rahisi na salama,bali unasaidia kupunguza gharama za maisha kwani nusu kilo ya maharage kwa kupikia umeme inagharimu kiasi cha Sh.200 ikilinganishwa na 1,200 kwa mkaa,kulinda mazingira na kuboresha afya za wananchi hasa wanawake.
Alisema,vifaa vingi vinavyotumia umeme kwa sasa vimeboreshwa hivyo kuwezesha kutumika kwa umeme wa gharama ndogo katika matumizi mbalimbali tofauti na ilivyouwa awali.
“Kupitia wiki ya huduma kwa wateja,tuko katika soko hili la Bombambili kuwaelimisha wananchi faida mbalimbali za kutumia Brenda,majagi ya kuchemshia maji na majiko ili wasiogope na kuhofu juu ya gharama za kupika chakula kwa kutumia umeme,teknolojia ya majiko haya imeboreshwa tofauti na zamani”alisema Njiro.
Mariam Abdul wa kitengo cha usafirishaji cha Shirika hilo alisema,wakati wanaadhimisha wiki ya huduma kwa wateja wameona wafanye maenesho ya kutangaza matumizi ya nishati safi na kuhamasisha wananchi watumie majiko ya umeme kwa kupikia na shughuli mbalimbali.
Alisema,watu wengi wamezoea kutumia umeme kwa ajili ya Televisheni,friji,feni na vitu vingine lakini kwenye kupika wanadhani kutumia umeme ni gharama kubwa jambo ambalo sio sahihi.
“Unakuta mtu anatumia umeme kwa ajili ya kuchaji simu,feni,friji na vifaa vingine lakini kwenye kupika anadhani gharama zake ni kubwa sana,kwa hiyo katika wiki ya huduma kwa wateja Tanesco tumeona tuje kuwaelimisha wateja wetu umuhimu wa kutumia umeme kwa ajili ya kupikia kwani gharama zake ni rahisi na nafuu sana”alisema Mariam.
Aidha alisema,kupika kwa kutumia umeme ni salama na safi tofauti na mtu anayetumia mkaa na kuni na kuwasisitiza wananchi kuanza kutumia umeme kwa ajili ya kupikia.
Mfanyabiashara wa chakula katika soko la Bombambili Mariam Mfaume alisema,kuna tofauti kubwa kati ya jiko la umeme na mkaa kwenye kupika kwani kutumia umeme chakula kinaiva kwa muda mfupi na mpishi hachafuki.