
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetoa taarifa rasmi likibainisha kuwa mwongozo wa kupima na kuthibitisha jinsia za wachezaji wa kike utaanza kutumika rasmi kuanzia msimu wa 2026/27.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, TFF imesema kuwa kwa msimu huu wa 2025/26 hakuna mchezaji yeyote atakayepimwa, huku likisisitiza kwamba maandalizi ya utekelezaji wa mwongozo huo bado yanaendelea kufanyiwa kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa michezo na afya.
“Tunaendelea kuandaa mfumo sahihi, wenye kuzingatia maadili, haki za binadamu na kanuni za michezo ya kimataifa kabla ya utekelezaji kuanza msimu ujao,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
Uamuzi huo unakuja baada ya mijadala mikubwa kuibuka wiki kadhaa zilizopita, kufuatia agizo la awali lililotaka baadhi ya wachezaji wa kike kupimwa ili kuthibitisha jinsia zao.
TFF imesisitiza kuwa lengo la mwongozo huo ni kuimarisha uwazi na usawa wa ushindani katika soka la wanawake, sambamba na kulinda heshima na utu wa wachezaji wote wanaoshiriki ligi hiyo.