Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imeelezea dhamira yake ya kushirikiana kwa karibu na Jukwaa la Watendaji Wakuu (CEO Roundtable of Tanzania -CEOrt) katika kuendeleza mijadala yenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kurahisisha utekelezaji wa sheria za kodi kupitia sekta binafsi ili kuongeza mapato kwa maendeleo ya nchi.
Haya yamejitokeza katika kikao cha ngazi ya juu kilichoandaliwa na CEOrt, kilichowakutanisha viongozi waandamizi wa TRA, wanachama wa CEOrt, wataalamu wa masuala ya kodi na wawakilishi waandamizi wa serikali kwa ajili ya kujadili namna ya kuimarisha usimamizi wa kodi, kuimarisha ushirikiano, na kubaini maeneo ya kipaumbele ya marekebisho ya sera kwa ajili ya kuvutia uwekezaji na kukuza uchumi.
Akihudhuria kama Mgeni Rasmi na Mzungumzaji Mkuu, Kamishna Mkuu wa TRA, Mhe. Yusuph J. Mwenda, alitoa hotuba iliyoongozwa na kaulimbiu “Kujenga Mazingira Imara ya Kodi kwa Maono ya Maendeleo ya Tanzania 2050.”
Alisisitiza kuwa TRA imeanza kubadili mkakati wake kutoka kuwa taasisi ya kutumia nguvu na badala yake kuweka mazingira rafiki katika uboreshaji wa huduma ili kuwezesha ukuaji wa biashara na uundaji wa ajira.
“Mwelekeo wetu sasa unalenga kuwezesha badala ya kulazimisha. Mfumo wa kisasa wa kodi unatakiwa kuirahisishia biashara kutekeleza wajibu wake, kukua na kuajiri.
” Tunapolenga Maono ya Dira ya 2050, ushirikiano na sekta binafsi kupitia CEOrt ni msingi wa kujenga uchumi jumuishi na imara,” alisema Kamishina. Mwenda.
Aidha, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha mazingira ya biashara yanakuwa bora na endelevu.
“Ndiyo sababu Rais alianzisha Kamati ya Kitaifa ya Mapitio ya Kodi, ambayo baadhi ya wajumbe wake ni wanachama wa CEOrt, kwa ajili ya kusaidia kuleta mageuzi chanya katika uchumi wa taifa,” alisema.
Akifungua kikao hicho, Mjumbe wa Bodi ya CEOrt, Bw. David Nchimbi, alieleza umuhimu wa kuwa na mifumo ya kodi iliyo wazi na inayotabirika katika kuongeza imani ya wawekezaji na kuleta maendeleo endelevu.
“Mkutano huu ni jukwaa muhimu kwa mazungumzo ya wazi kati ya serikali na sekta binafsi, jambo ambalo linasaidia kufanikisha marekebisho ya sera zinazokubaliana na uhalisia wa biashara,” alisema Bw. Nchimbi.
Kikao hicho kilichoendeshwa na Mwenyekiti wa Bodi ya CEOrt, Bw. David Tarimo, kilijikita katika kutafuta suluhisho la makadirio ya kodi, kurahisisha uzingatiaji wa sheria, na kujenga imani ya pamoja kati ya TRA na jamii ya wafanyabiashara.
Alieleza kuwa mjadala huo ni muhimu, kwani wanachama wa CEOrt —inayojumuisha taasisi na makampuni 230 kutoka sekta mbalimbali — ni miongoni mwa walipa kodi wakuu wanaochangia maendeleo ya nchi.
“CEOrt itaendelea kuwa kiunganishi muhimu katika kuendesha majadiliano yenye ushahidi kati ya sekta binafsi na taasisi za serikali.
Mazungumzo ya dhati na yenye kuheshimiana yanawezesha upatikanaji wa suluhisho ambalo linaimarisha ufanisi wa utawala pamoja na ustawi wa biashara,” alisema Bw. Tarimo.
Washiriki walikaribisha hatua ya TRA katika mageuzi ya kidijitali na kusisitiza umuhimu wa tafsiri ya sheria za kodi kufanywa kwa namna thabiti na sawa katika sekta zote.
Kikao hicho kimefanyika katika kipindi ambacho takwimu za mapato zinaonyesha mafanikio.
TRA imeripoti kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/26, makusanyo ya mapato ya ndani yalifikia Shilingi trilioni 8.97, na hivyo kuzidi lengo kwa zaidi ya asilimia 6 — jambo linaloashiria ufanisi unaoongezeka wa mageuzi ya sasa na fursa ya kuimarisha mapato bila kuathiri ustawi wa biashara.
CEOrt inapoadhimisha miaka 25 ya kuongoza kwa kukuza sekta binafsi, mkutano huo umeonesha tena dhamira ya kuendeleza mijadala ya kitaifa yenye tija katika maeneo ya sera za fedha, utawala bora na maendeleo endelevu.
Mmoja wa wanachama wa CEOrt, Bi. Jackline Woiso, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa MultiChoice Tanzania, alielezea matumaini yake juu ya kuendelea kushirikiana na TRA na taasisi nyingine katika kujenga mazingira wezeshi kwa uwekezaji na ukuaji wa uchumi jumuishi na endelevu.