Na Daudi Nyingo
Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imeendelea kuimarisha uhusiano na wateja wake kupitia maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, yanayofanyika kitaifa kuanzia tarehe 6 hadi 11 Oktoba 2025, kwa kaulimbiu isemayo “Huduma Bora za TVLA ni Haki ya kila mteja.”
kuadhimisha wiki hiyo, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TVLA, Bw. Furaha Kabuje, alifanya ziara maalum katika baadhi ya maduka yanayouza bidhaa za TVLA jijini Dar es Salaam Oktoba 09, 2025 kwa lengo la kusikiliza maoni ya wadau mbalimbali hususan wauzaji wa bidhaa na wanufaika na huduma zinazotolewa na Wakala.
Akizungumza katika moja ya maduka hayo, Bw. Kabuje alisema kuwa TVLA itaendelea kuzingatia ubora wa bidhaa zake hususan chanjo za mifugo ili kuhakikisha zinaimarisha afya za mifugo yetu nchini.
“Lengo letu ni kuhakikisha kila mteja wa TVLA anapata bidhaa na huduma bora, salama na yenye ubora unaokidhi mahitaji ya sekta ya mifugo nchini. Tunathamini sana maoni kutoka kwa wadau wetu kwa kuwa ndiyo kioo chetu katika kuboresha huduma zetu kila siku,” alisema Bw. Kabuje.
Aidha, aliwahakikishia wauzaji wa bidhaa hizo kwamba Wakala itaendelea kushirikiana nao kwa karibu zaidi katika maeneo ya usambazaji, elimu kwa wateja na upatikanaji wa bidhaa kwa wakati, sambamba na kuboresha mifumo ya mawasiliano kati ya ofisi za TVLA na wateja wake.
Kwa upande wao, baadhi ya wauzaji wa bidhaa za TVLA waliotembelewa mkoa wa Dar Es Salaam na Pwani walitoa pongezi kwa Wakala kwa hatua ya kuwafikia moja kwa moja na kusikiliza maoni yao, wakibainisha kuwa hiyo ni njia bora ya kujenga mahusiano endelevu na wateja.
waliongeza kuwa wanaishukuru TVLA kwa kuwatembelewa na vilevile ubora wa chanjo wanazozizalisha, lakini wangependa kuona upatikanaji wa baadhi ya bidhaa ukiimarishwa zaidi pamoja na kuimarishwa kwa mawasiliano ya moja kwa moja kati ya wauzaji na ofisi za Wakala ili kupata taarifa za bidhaa sahihi pamoja na upatikanaji wa bidhaa kwa wakati.
Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya TVLA katika kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa mawasiliano na wateja wake kote nchini. Kupitia Wiki ya Huduma kwa Wateja, Wakala inajenga mazingira rafiki ya kujifunza kutoka kwa wadau wake na kuendelea kutoa huduma bora kwa maendeleo ya sekta ya mifugo nchini.