
Na Mwandishi Wetu
UJUMBE wa wageni kutoka Japani umetembelea kiwanda cha mavazi kilichopo Mabibo, Ubungo jijini Dar es Salaam,Oktoba 08, 2025 kwa lengo la kujifunza zaidi kuhusu mazingira ya biashara na fursa za uwekezaji nchini Tanzania.
Ujumbe huo ulihusisha ofisi ya Ubalozi wa Japani nchini Tanzania, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japani (JICA) pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kijapani (Japanese Chamber of Commerce), wakiwemo baadhi ya wafanyabiashara binafsi kutoka kampuni mbalimbali za Japani.
Ziara hiyo ililenga kuangalia kwa vitendo maeneo maalum ya uwekezaji yanayosimamiwa na mamlaka hiyo pamoja na kubaini sekta zenye fursa kubwa za biashara, hususan katika sekta ya viwanda na biashara.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wawekezaji wa TISEZA, James Maziku, alisema ujio wa sekta binafsi za Japani unaonyesha wazi kuongezeka kwa hamasa ya wawekezaji wa Japani kuwekeza nchini, hasa katika miradi inayochangia ajira na ukuaji wa uchumi wa viwanda.
“Tumeamua kufungua ukurasa mpya wa majadiliano ya kibiashara ili kuwaeleza wawekezaji fursa tulizonazo kwa undani zaidi. Tunataka maeneo haya yaliyotengwa kwa uwekezaji yageuzwe kuwa miradi halisi itakayowanufaisha wananchi wote,” alisema Maziku.
Kwa upande wake, Katibu wa Maendeleo ya Kiuchumi kutoka Ubalozi wa Japani, Jin Hashimoto, alisema lengo kuu la ujio huo ni kujifunza zaidi kuhusu sekta za viwanda zilizopo nchini Tanzania.
“Nimekuwa nikiishi Tanzania kwa miaka miwili, na hii ni mara yangu ya kwanza kushiriki katika tukio kama hili. Ninaamini maendeleo ya viwanda hapa Tanzania yanatoa fursa nzuri kwa jumuiya ya wafanyabiashara wa Kijapani,” alisema Hashimoto.
Kwa upande wa Ryutaro Miyamoto kutoka kampuni ya Sumitomo Corporation ya Japani, alisema kuwa ujio huo unalenga kuelewa mazingira ya biashara na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Japani.
“Tunaendelea kujitahidi kujifunza zaidi kuhusu mazingira ya biashara kwa ujumla hapa Tanzania. Kwa kweli, uhusiano wa kiuchumi kati ya Japani na Tanzania unaendelea kukua,” alisema Miyamoto.
Aidha, alikumbusha kuwa mwaka jana mwezi Mei, Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambacho sasa kinajulikana kama TISEZA alitembelea Japani kushiriki katika semina muhimu ya biashara, na mwaka huu Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani alitembelea Tanzania kwa ajili ya mashauriano ya kuimarisha zaidi mazingira ya uwekezaji.
Vilevile, wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa, alipotembelea Japani kushiriki maandalizi ya Osaka Expo, wajumbe wa T-SEZA pia walitembelea Japani na kufanya mazungumzo na wawekezaji.
Kwa mujibu wa viongozi hao, hatua hizi zote zinaongeza kasi ya ushirikiano wa biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Japani, huku sekta ya viwanda vya mavazi ikionekana kuwa miongoni mwa maeneo yenye mvuto mkubwa kwa wawekezaji kutoka nchini Japani.
Matukio mbalimbali wakati wa Wajapani walipotembelea kiwanda cha Mavazi cha Mabibo, Ubungo jijini Dar es Salaam Oktoba 08, 2025.