Na Mwandishi Wetu- Itilima
Wananchi wa vijiji vya Nyantugutu, Lung’wa na Nding’ho vya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu wameipongeza Serikali kwa kuunda na kuboresha mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za wanyamapori wakali na waharibifu (Problem animal information system- PAIS) ambao umerahisisha malipo ya kifuta jasho/machozi pindi madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu yanapotokea kwa wananchi.
Hayo yamesemwa na Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Ndi’hgo , Bi. Salome Kambona katika mkutano wa hadhara wa kuelimisha wananchi namna ya kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu uliofanyika kijiji cha Ndi’hgo ,Wilaya ya Itilima leo Oktoba 9, 2025.
“Tunaishukuru Serikali kwa mfumo huu ambao ndani ya siku saba mwananchi atatakiwa awe ametoa taarifa ya madhara yaliyotokana na mnyamapori ili aweze kulipwa” amesema Bi.Salome.
Naye, Mkazi wa Kijiji cha Nyantugutu, Bw. Mosses Saguda amesema mfumo wa PAIS umepunguza urasimu na usumbufu wa malipo.
“Tunaishukuru Serikali kwa utaratibu mpya wa mfumo wa malipo ya kifuta jasho/machozi kwani hauna usumbufu wowote na tunalipwa kwa simu au benki tofauti na awali tulikuwa tunakaa mwaka bila kulipwa” amesema Bw. Saguda.
Aidha, ameiomba Serikali kuangalia namna ya kuweka utaratibu wa malipo ya kifuta jasho kwa wananchi wanaoharibiwa mazao yakiwa ghalani.
Akizungumza kuhusu elimu hiyo kwa wananchi, Afisa Wanyamapori Mkuu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Nassoro Wawa amesema matarajio ya Serikali baada ya mafunzo hayo ni kwamba wananchi wamepata uelewa jinsi ya kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na kujua sheria, kanuni na taratibu za kufuata ili kumiliki nyara za Serikali.
“Pia nimewaeleza wananchi kuwa sheria zinaruhusu kuwekeza katika sekta ya wanyamapori hususan kuanzisha bucha za nyamapori, bustani, mashamba na ranchi za wanyamapori ili waweze kujipatia vipato” amesisitiza Bw. Wawa.
Elimu hiyo imetolewa Mkoani humo kufuatia matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu hususan tembo,fisi, mamba na viboko.