
Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuwekeza katika kujenga nguvu kazi yenye ujuzi wa kisasa, ubunifu na maadili, ili iweze kushindana katika soko la ajira la kikanda na kimataifa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Oktoba 11, 2025 katika ufunguzi wa Kongamano la Kumbukizi ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere lililofanyika katika Ukumbi wa Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Amesema kuwa ubora wa watu ndio msingi wa mafanikio ya Taifa lolote duniani.
“Mafanikio ya taifa letu katika miaka ijayo yatategemea ubora wa watu wake. Msingi wa maendeleo ni watu wenye ujuzi, ubunifu, na maadili. Tuweke mbele elimu bora, ujuzi, ubunifu na uzalendo kama silaha za kujenga taifa lenye ustawi, amani na maendeleo jumuishi,” amesema Majaliwa.
Amesema Serikali imekuwa ikitekeleza mipango ya kimkakati ya kukuza ujuzi kwa wananchi kupitia programu mbalimbali, ikiwemo kuanzishwa kwa vyuo vya elimu ya ufundi (VETA) katika kila wilaya, na Programu ya Taifa ya Maendeleo ya Ujuzi (National Skills Development Programme) inayolenga kuwajengea vijana ujuzi katika sekta za kilimo, viwanda, teknolojia, nishati na huduma.
“Lengo letu ni kuandaa kizazi cha vijana kinachoweza kuchochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla. Hatuwezi kujenga uchumi wa kisasa bila nguvu kazi yenye ujuzi unaoendana na mahitaji ya sasa ya dunia,” ameongeza Waziri Mkuu Majaliwa
Aidha, aliwaalika vyuo vikuu, taasisi za utafiti, Tume ya Sayansi na Teknolojia, sekta binafsi na vijana kote nchini kushirikiana katika kutekeleza kwa vitendo malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ikiwemo kuboresha ubunifu na kuhamasisha matumizi ya teknolojia katika sekta mbalimbali.
Majaliwa alizitaka sekta binafsi na mashirika ya umma kuanzisha programu za mafunzo kwa vitendo (internship) katika maeneo ya kazi, ili kukuza stadi za kazi kwa vijana wanaomaliza vyuo na kuwasaidia kujiandaa kwa ajira.
Mkurugenzi wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, amesema kuwa maendeleo ya Taifa na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa nguvu kazi yenye ujuzi na ubora, ambayo ndiyo urithi halisi wa fikra za Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kafulila amesema kuwa mwanafunzi wa chuo kikuu anapaswa kuwa kama trekta, akimaanisha mtu mwenye nguvu, maarifa na uwezo wa kusukuma maendeleo ya Taifa.
“Ni miaka 57 tangu tuanze safari ya kujitegemea, bado tunapaswa kuendelea kuwa waanzilishi wa dunia mpya. Dunia ya leo inategemea ubora wa nguvu kazi tuliyonayo, ndiyo kipimo cha jinsi Taifa linavyoweza kupambana na changamoto na kufikia maendeleo,” amesema Kafulila
Amefafanua kuwa utajiri wa Taifa haupimwi kwa wingi wa maliasili pekee, bali kwa kiwango cha elimu na ubora wa nguvu kazi iliyopo.
“Ushahidi uko wazi. Kuna mataifa yenye maliasili nyingi lakini ni masikini, na yapo yasiyo na maliasili lakini ni matajiri. Hii ina maana kuwa chanzo cha utajiri wa mataifa yote ni elimu na ubora wa nguvu kazi, bila kujali kama una au huna rasilimali asilia,” amesisitiza.
“Mwekezaji anaweza kusita kuwekeza endapo ubora wa wataalamu katika sekta binafsi au ya umma hautoshi. Ndiyo maana Serikali imeendelea kuboresha mitaala ya elimu ili iendane na mahitaji ya soko la ajira, na kuhakikisha vijana wanapata maarifa yanayohitajika katika maeneo husika,” ameongeza.
Kwa mujibu wa Kafulila, hatua hizo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kujenga uchumi wa viwanda na ubunifu, ambapo nguvu kazi bora itakuwa nguzo ya ushindani wa Taifa katika soko la kikanda na kimataifa.
Kwa upande wa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Daniel Mushi, amesema Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika kukuza nguvu kazi ya Taifa kupitia miradi ya elimu, ujenzi wa miundombinu, utafiti, na mafunzo ya vitendo.
“Serikali imeongeza fedha kwa ajili ya kuboresha mifumo ya upangaji wa mikopo ya elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ili kuhakikisha kila mwanafunzi mwenye uwezo kitaaluma, bila kujali hali ya kifedha, anapata fursa ya kusoma,” amesema Prof. Mushi.
Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, Profesa Alexander Makulilo, amesema kongamano hilo lina lengo la kuenzi urithi wa Mwalimu Nyerere katika kukuza rasilimali watu, kubaini mbinu za kimkakati za kujenga nguvu kazi yenye ujuzi, na kuchochea majadiliano baina ya wadau kuhusu sera na ubunifu unaoendana na Dira ya Taifa ya 2050.
MADA KATIKA KONGAMANO HILO NI; Nguvu Kazi Yenye Ujuzi kwa Maendeleo ya Taifa: Kwa Kuendeleza Urithi wa Mwalimu Nyerere Kuelekea Dira ya 2050
Matukio mbalimbali katika uzinduzi wa Kongamano la kumuenzi Mwalimu Nyerere lililifanyika jijini Dar Es Salaam leo Oktoba 11, 2025.