NA JOHN BUKUKU – KAHAMA, SHINYANGA
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa Wilaya ya Kahama inatarajiwa kupata msukumo mkubwa wa kiuchumi kufuatia ujenzi wa viwanda vipya katika eneo la mgodi wa Buzwagi, baada ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo ya kuhakikisha eneo hilo linabaki likitumika kwa shughuli za kibiashara.
Akizungumza Oktoba 11, 2025, katika Viwanja vya Magufuli wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, wakati wa muendelezo wa kampeni za Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mavunde alisema wawekezaji wameonyesha nia ya kuanzisha viwanda sita vipya vitakavyotoa ajira kwa wananchi na kuongeza mapato ya Halmashauri. Hatua hiyo inatarajiwa kuchochea ukuaji wa uchumi wa Kahama na taifa kwa ujumla.
Amesema kuwa Wilaya ya Kahama ina shughuli kuu mbili za kiuchumi ambazo ni kilimo na madini. Ili kusaidia wachimbaji wadogo, serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 9 kwa ajili ya kununua mashine za kuchoronga madini kote nchini. Hadi sasa, mashine 16 zimewasili Kahama kusaidia wachimbaji wadogo, ambapo gharama ya kukodi mashine moja kwa kuchimba mita 100 ni shilingi milioni 23. Amesema wachimbaji wadogo hulipa shilingi milioni 10 pekee kwa mita hizo, na tofauti iliyobaki hulipwa na serikali kama ruzuku kwao.
Aidha, Waziri Mavunde amefafanua kuwa jumla ya leseni 2,648 za wachimbaji wadogo zimefutwa, huku Wilaya ya Kahama ikitoa leseni 1,375 mpya, ikiwemo kwa kikundi cha TAWOMA ambacho huchangia zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa mwaka katika mapato ya Halmashauri. Kikundi hicho pia kimejenga zahanati na nyumba za madaktari kama sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii.
Amebainisha kuwa wachimbaji wadogo wanapaswa kuepuka uchorongaji wa bahati nasibu, na badala yake wafuate maelekezo ya serikali ambayo yanahusisha matumizi ya teknolojia, ikiwemo helikopta maalum inayoweza kuchunguza madini hadi umbali wa kilometa moja chini ya ardhi. Amesema pia kuwa ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 73 kutoka Kahama hadi mpaka wa Kakola unaendelea, na baadaye barabara hiyo itaunganisha mkoa wa Shinyanga na Geita, jambo litakalorahisisha usafiri wa wachimbaji na biashara kwa ujumla.
Vilevile, ameeleza kuwa serikali imeweka kanuni mpya kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata haki zao, ikiwemo mgawanyo wa mapato kwa uwiano wa asilimia 30 kwa wachimbaji wadogo na asilimia 70 kwa serikali. Sheria ya Madini, kifungu cha 8, inakataza wageni kuingia kwenye machimbo ya wachimbaji wadogo, huku kifungu cha 3 kikielekeza kuwepo kwa mikataba rasmi kati ya pande husika.
Amesisitiza kuwa sekta ya madini imeendelea kuwa nguzo muhimu ya uchumi wa Tanzania, ambapo jumla ya tani 12 za dhahabu zimeuzwa hadi sasa, ikiwemo dhahabu inayozalishwa katika Wilaya ya Kahama, ambayo imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza pato la taifa.