

Mgombea wa nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 12 Oktoba 2025, ameendelea na ziara yake ya kampeni katika Mkoa wa Geita, akifanya mkutano mkubwa wa hadhara katika kata ya Masumbwe, wilayani Mbogwe.
Baada ya kuhutubia umati mkubwa wa wananchi waliokuwa wamefurika uwanjani, Dkt. Samia alipungia mkono wananchi kwa furaha kama ishara ya shukrani kwa mapokezi makubwa na hamasa waliyoonyesha.
Katika hotuba yake, Dkt. Samia alisisitiza dhamira ya CCM kuendeleza utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayogusa moja kwa moja maisha ya wananchi, ikiwemo miundombinu ya barabara, elimu, afya na maji safi. Pia aliahidi kuendeleza jitihada za kuimarisha uchumi wa wananchi kupitia sekta za kilimo, madini, na biashara ndogo ndogo.
Wananchi wa Masumbwe walionekana na hamasa kubwa, wakipeperusha bendera za kijani na njano huku wakipiga nderemo na vifijo wakimsikiliza kiongozi huyo wa taifa.
Ziara hii ni sehemu ya muendelezo wa kampeni za CCM kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo Dkt. Samia ameendelea kusisitiza amani, umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania wote bila kujali tofauti zao za kisiasa.
#BREAKING: WAGOMBEA UDIWANI 7 wa CCM WATENGULIWA na TUME ya UCHAGUZI – SABABU ZATAJWA…