Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Geita
MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amewakumbusha vijana nchini kuwa nchi inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ipo moja peke yake na tangu imeundwa imepigana vita moja na tu Idi Amin na kwa sababu aliichokoza.
Amesema lakini kwa miaka yote nchi ipo salama, ina amani na kwamba wao walikuwa wadogo wamekuzwa kwenye amani mpaka wamekuwa wakubwa wanaendesha nchi hiyo bado wanalinda amani.
Dk.Samia ameyasema hayo leo Oktoba 12,2025 alipokuwa akizungumza na maelfu ya wananchi wa eneo la Runzewe katika Wilaya ya Bukombe mkoani Geita akiwa katika mkutano wa kampeni kuomba kura kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.
“Vijana twendeni tukalinde amani yetu, tusikubali kwa hali yeyote kushawishiwa kuharibu amani yetu. Hamtakwenda kwenye kuchimba, hamtakwenda kwenye muziki, hamtafanya chochote amani ikiharibika.
“Wakati nakuja huku (Bukombe)nilisimama Kahama ambako kuna mchanganyiko wa watu kutoka nchi jirani wote wapo pale wamefuata biashara, wamefuata maisha, wamefuata amani.
“Mkiharibu ninyi kwenu kama wale wanakuja huku nyie mtakwenda mtakwenda wapi. Hamtapata pa kukimbilia. Pakukimbilia na hapa kwetu. Niwaombe kwa njia yeyote ile asije mtu akasema fanyeni hiki fanyeni hiki mkavuruga amani ya nchi yetu na mkaharibu sifa nzuri ya nchi yetu.”
Dk.Samia amesema nchi ya Tanzania inaheshimiwa sana na sifa zake amani yake kwa maendeleo yake na kwa maumbile yake. “Kwa hiyo niwasihi sana vijana wangu tuwe wazalendo tuipende nchi yetu tusije tukarubuniwa kwa namna yeyote tukaharibu nchi yetu.
Katika hatua nyingine Dk.Samia amesema jambo la farauja ni kwamba Mbunge wao ambaye pia ni Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk.Mashaka Biteko aliwahi kumwambia vijana hawana sehemu ya michezo.
“Tutakubaliana kuunga mkono nguvu serikali tukaenda na sekta binafsi tunajenga kiwanja kikubwa cha kisasa cha michezo Ushirombo.
“Kiwanja kizuri sana cha michezo ambacho Bukombe itaingia kwenye ramani ya wilaya ambazo kama mechi za ligi kuu ya Tanzania Bukombe kutakuwa na kiwanja.
“Hiyo ni zawadi ya serikali yenu kwa vijana tunawapa kazi za kiuchumi lakini tunawapa maeneo ya kufanyia michezo na kuburudika.
Serikali tunawapenda sana na tunawaomba nanyinyi muipende nchi yenu.”