

Nyota wa Paris Saint-Germain, Ousmane Dembele, ameiomba klabu yake kumpa mkataba mpya na ongezeko la mshahara linalolingana na hadhi yake mpya kama mshindi wa Ballon d’Or 2025.
Kwa sasa Dembele analipwa takribani euro milioni 18 (shilingi bilioni 52 za Kitanzania) kwa mwaka na bado ana mkataba unaomfunga na PSG hadi mwaka 2028. Hata hivyo, baada ya mafanikio yake binafsi na ushindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, winga huyo wa Ufaransa anahisi ni wakati wa kutambuliwa kifedha.
Taarifa kutoka L’Équipe zinaeleza kuwa mkataba wa Dembele unaweza kuwa na kipengele cha nyongeza ya mshahara endapo atashinda Ballon d’Or jambo ambalo PSG inakanusha rasmi. Hata hivyo, wawakilishi wa Dembele wanataka klabu iheshimu kipengele hicho, wakisema mafanikio yake ni ishara tosha ya kuthibitisha ubora wake duniani.
Viongozi wa PSG, wakiongozwa na Nasser Al-Khelaifi na mkurugenzi wa michezo Luis Campos, wameweka sera kali ya kifedha ili kuepuka makosa ya enzi za Neymar, Kylian Mbappe na Lionel Messi, ambapo mishahara mikubwa ilisababisha changamoto za usawa wa kikosi na sheria za Financial Fair Play.
Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV — usisahau ku-like, ku-comment na ku-subscribe ili uendelee kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.